PROF. MKUMBO UCHUMI UMEBAKI IMARA LICHA YA MDORORO WA DUNIA
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na
Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amehitimisha mjadala wa wabunge kuhusu hali
ya uchumi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2025/2026, akisisitiza kuwa
uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara na himilivu katikati ya mdororo wa
uchumi duniani
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma leo, Prof.
Mkumbo alitumia takwimu za ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) na Mfumuko wa Bei
kuonesha kuwa Tanzania inafanya vizuri ikilinganishwa na wastani wa kimataifa
na hata kikanda
Akifafanua zaidi, Waziri Mkumbo alieleza kuwa
wakati dunia na kanda zikikabiliwa na changamoto za kiuchumi, Tanzania
imefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei, ambao ulikuwa asilimia 3.1 mwaka 2024,the
kiwango ambacho ni chini sana ya wastani wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) cha asilimia 54.6 na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) cha
asilimia 23.
Aidha, alibainisha kuwa Pato la Taifa lilikua
kwa asilimia 5.1 mwaka 2023 na linakadiriwa kukua kwa asilimia 5.5 mwaka 2024,
viwango ambavyo ni vya juu kuliko wastani wa dunia (3.3%) na nchi za SADC
(3.1%)
"Alisema siri ya ustahimilivu huu ni mseto
wa vyanzo vya uchumi, vikiwemo kilimo, utalii, madini, na ujenzi"
Prof. Mkumbo aliorodhesha mafanikio makubwa
yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu
Hassan, ambayo yamechangiwa na bajeti zilizopitishwa na Bunge
Alitaja uwekezaji mkubwa katika huduma za jamii,
ikiwemo matumizi
ya Shilingi trioni 1.3 kwa ajili ya elimu bila ada kuanzia shule ya msingi hadi
kidato cha sita, na Shilingi trioni 2.7 zilizotolewa kama mikopo kwa wanafunzi
wa elimu ya juu.
Pia aligusia mpango wa Serikali wa kutekeleza
Bima ya Afya kwa Wote, ambao umewekewa vyanzo vya mapato katika bajeti ya mwaka
huu
Akiwajibu wale wanaokosoa na kutoona mafanikio
yaliyofikiwa, Waziri Mkumbo alirejelea maneno ya Rais wa Awamu ya Pili, Hayati
Ali Hassan Mwinyi, aliyewahi kusema, "...asiyeyaona maendeleo kwa sababu
macho ni magonjwa atege masikio asikilize haya tunayoyasema!"
Alisema ni muhimu kwa wananchi kutambua kazi
kubwa inayofanywa na Serikali ya CCM.
Katika hotuba yake, Waziri alikiri kuwa
maendeleo ni mchakato endelevu wenye mafanikio na changamoto, akitolea mfano wa
Mwalimu Nyerere ambaye alikiri na kusahihisha baadhi ya makosa yake ya kisera.
Alimsifu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa
kiongozi mwenye ujasiri wa kuendeleza mema, kusahihisha yaliyokosewa, na
kukabiliana na changamoto Mjadala wa mpango huo ulihitimishwa baada ya wabunge
97 kutoa michango yao.
Prof. Mkumbo alitoa shukrani kwa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Bajeti na kumpongeza Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba,
kwa kuwasilisha bajeti iliyopokelewa vizuri na wananchi na vyombo vya habari.
Alihitimisha kwa kuwataka wabunge kwenda
majimboni kuwaombea kura Rais Samia Suluhu Hassan na chama cha CCM katika
uchaguzi ujao.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Dkt. Tausi Kida akifuatiliali mjadala Bungeni jijini Dodoma leo, kabla ya kuhitimishwa kwa mjadala wa Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2025/26. Mjadala ulihitimishwa rasmi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.
No comments