Breaking News

WIZARA ZA KISEKTA ZAKUTANA KUJADILI AFUA ZA AFYA NA LISHE SHULENI

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Otilia Gowelle akizungumza katika Kikao  cha Kamati ya Wataalam cha Ushauri wa Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya na Lishe Shuleni (TAC),   mkoani Morogoro.
................................

Na.Elimu ya Afya, Morogoro.

Wizara za Kisekta zimekutana mkoani Morogoro  kujadili utekelezaji wa  Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya  na Lishe Shuleni.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao  cha Kamati ya Wataalam cha Ushauri wa Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya na Lishe Shuleni (TAC),   mkoani Morogoro,  Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Otilia Gowelle amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na uzalishaji wa chakula shuleni pamoja na mashamba darasa ili kuwapa uelewa katika masomo darasani.

"Kuna umuhimu mkubwa wa uzalishaji wa chakula shuleni hivyo kupitia kikao hiki ni vyema tuweke mikakati ya pamoja ili afua za afya na lishe shuleni ziwe imara zaidi," amesema Dkt. Gowelle.

Aidha, Dkt. Gowelle amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta, Taasisi ya Elimu Tanzania na Engender Health imefanikiwa kufanya tathmini ya ujumuishi wa maudhui yanayopendekezwa kimataifa katika mada za afya, lishe na ustawi ndani ya mtaala wa elimu ya Stashahada ya ualimu.

Kwa upande wake Mratibu wa dawati la Afya moja  kutoka  Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Salum Manyata  amesema kuna umuhimu  wa ushirikiano kwa  Wizara  zote za Kisekta.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya na Lishe afya Shuleni.

Naye Mwakilishi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bakari Maghalawa  amesema  Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya na lishe shuleni una mchango mkubwa kwani   Wizara za Kisekta zinakaa na kuweka mikakati ya pamoja katika kuhakikisha afua za afya na lishe zinatekelezwa ipasavyo maeneo ya shule.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya  Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Sebastian Kitiku amesema katika kumwezesha mtoto inapaswa kuwa na mikakati ya pamoja.

"Huwezi kumwendeleza mtoto peke yako, na tunaposema ukuaji wa mtoto inajumuisha na uwezo wa kufikiri
na ili aweze kuwa na uelewa zaidi lazima apate lishe, hivyo ni lazima tujumuike pamoja katika kuhakikisha eneo la afya na lishe shuleni linaimarika," amesema  Dkt. Kitiku.

Mwakilishi wa  Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma ambaye pia ni Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Afya na Lishe Shuleni kutoka Wizara ya Afya Bi.Beauty Mwambebule amesema  uanzishaji wa klabu za afya shuleni zitakuwa na tija kubwa katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya na Lishe shuleni.

Wizara za Kisekta zilizokutana ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Rais TAMISEMI, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Elimu, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Mifugo na Wizara ya Afya.


 

No comments