MKUU WA WILAYA YA MLELE AANZA ZIARA YA SIKU TANO MPIMBWE MKOA WA RUKWA
Mkuu wa Wilaya ya Mlele leo Jumatatu, tarehe 21 Julai 2025, ameanza ziara ya siku tano kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo. Ziara hii imeanza kwa kutembelea Mlima wa Lyamba Lyamfipa katika kata za Majimoto, Mamba na Kasansa ili kujionea hali ya mazingira na fursa zilizopo.
Kesho Jumanne tarehe 22 Julai, Mkuu huyo wa wilaya atatembelea Ziwa Rukwa asubuhi na mchana atagawa hati za ardhi katika vijiji vya Mirumba na Luchima. Jumatano tarehe 23 Julai, atagawa vyeti kwa wahitimu eneo la Watusimba asubuhi, kisha ataongoza tukio la ugawaji wa hundi za mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi vya kina mama, vijana na watu wenye ulemavu.
Alhamisi tarehe 24 Julai, Mkuu wa Wilaya atakutana na watemi, viongozi wa sungusungu na waganga wa jadi asubuhi, pamoja na kufanya mkutano na wananchi kuhusu mrejesho wa bajeti na taarifa za umma za Halmashauri ya Mpimbwe. Ziara hiyo itahitimishwa Ijumaa tarehe 25 Julai kwa kikao na watendaji wa serikali pamoja na wadau wa lishe mchana.
Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe imesema ziara hii inalenga kuimarisha ushirikiano na uwajibikaji kwa viongozi na wananchi, huku ikisisitiza kaulimbiu yao inayosema, “ kazi na utu, tunasonga mbele.
No comments