SINGIDA WAOMBWA KUSHIRIKIANA KUTOKOMEZA UKEKETAJI
Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Hospitali ya Rufaa Mandewa Mkoa wa Singida, Shukuru Mbago akitoa elimu ya kupinga vitendo vya ukeketaji katika mnada uliofanyika Julai 9, 2025 Kijiji cha Ughandi Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
.......................................
Dotto Mwaibale na Philemon Solomon, Singida
SINGIDA WAOMBWA KUSHIRIKIANA KUTOKOMEZA UKEKETAJI
JAMII Mkoa wa Singida imeombwa kushirikiana ili kutokomeza
vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto hasa vya ukeketaji.
Ombi hilo limetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Hospitali ya Rufaa Mandewa Mkoa wa Singida, Shukuru Mbago wakati wa utoaji elimu ya kupinga vitendo vya ukeketaji katika mnada uliofanyika Julai 9, 2025 Kijiji cha Ughandi kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Mbago alisema wahanga wakuu wa vitendo hivyo vya ukeketwaji ni wasichana na watoto na kuwa wanakutana na madhira hayo kutokana na kutokuwa na maamuzi ya kuvikataa au kuvikubali kutokana na wazazi hama walezi wa watoto hao kuwa ndio wenye uamuzi wa kufanya hivyo.
“ Wahanga wa vitendo hivi wamekuwa wakipata madhara makubwa
ambayo ni ya kiakili hasa pale atakapojijua yupo tofauti na wenzake kutokana
kuondolewa sehemu ya mwili wake hivyo kumfanya kuwa na msongo na kujichukia
mwenyewe na kuwalaumu waliomfanyia kitendo hicho.
Alisema mhanga huyo akiwa mkubwa anaweza kupata na hali fulani
ambayo siyo nzuri hasa baada ya kubaini kuwa katika mwili wake kuna baadhi ya
vitu vimetolewa na wenzake wanavyo jambo ambalo linamuumiza kiakili na kumfanya
alie kwa uchungu hata kujitenga na wenzake jambo ambalo siyo zuri.
“Hawa watoto wanapokuwa shuleni huwa wanaambiana kuhusu
maumbile yao sasa inapotokea amegundua yupo tofauti na wenzake linamuumiza sana
na ni kosa kisheria kwani ni ukatili wa kimwili ambao unamsababishia maumivu
makali” alisema Mbago.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya Singida, Felix
Maigo alisema lengo kubwa la mafunzo hayo ni kupata uelewa wa pamoja ili
kutokomeza vitendo vyote vya ukatili hasa ukeketaji dhidi ya wasichana na
watoto ambavyo vinakiuka haki ya msingi kwa kundi hilo.
Nujma Mdiwila Afisa Ustawi wa Jamii Singida anasema mhanga
wa kukeketwa ana kabiliwa na maumivu makubwa wakati wa kushiriki tendo la ndoa
na kuona kama ni mateso jambo ambalo linaweza kuvunja ndoa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ughandi, Rajabu Husseni aliishukuru
Serikali na Shirika hilo kwa ushirikiano mkubwa wenye lengo la kukabiliana na
vitendo hivyo ambavyo vimeanza kupungua baada ya jitihada kubwa kufanyika.
“Tunalishukuru shirika la WOWAP chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Fatma Hassan Toufiq, kwa kuwezesha utoaji wa mafunzo haya ambayo ni ya muhimu katika jamii yetu,” alisema Hussein.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Shirika hilo lisilo la Kiserikali la Women Wake-Up (WOWAP) lenye makao yake makuu Jijini Dodoma linalojishughulisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto na utoaji wa msaada wa kisheria bure kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani Singida.
Shirika hilo linatoa elimu hiyo kwa ufadhili wa Shirika la Women Action Against FGM (WAAF) la Japan ambapo linatekeleza mradi wa kupinga ukeketaji kwa kutoa elimu katika makundi ya jamii kwenye wilaya hiyo.
Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya Singida, Felix Maigo, akishiriki kutoa elimu hiyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ughandi, Rajabu Husseni aliishukuru Serikali na Shirika hilo kwa kuwapa elimu hiyo.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo wakiwa katika mnada huo wakati wa kutoa elimu hiyo.
Vipeperushi vya kupinga ukeketaji vikisomwa na washiriki wa mafunzo hayo
Majadiliano yakifanyika.
No comments