TAYOTA, SERIKALI KUKETI KUJADILI ULAWITI, UBAKAJI MKOA WA TANGA
Mkurugenzi wa Tayota, Bw. George Bwire
..........................................
Mashaka Kibaya,Tanga.
TAASISI ya Tanga Youth Talent Association (TAYOTA) kupitia mradi wa Tanga yetu unaohusika kupambana na ukatili wa kijinsia kwa watoto,vijana na wanawake,imejipanga kuketi na mamlaka za kisheria kujadiliana juu ya changamoto zilizopo katika kushughulikia kesi za ubakaji na ulawiti.
Katika taarifa yake, aliyoitoa jana kwa Waandishi wa habari Jijini Tanga, Mkurugenzi wa TAYOTA,George Bwire alisema, taasisi hiyo imepata mradi wa miezi 13 na wamejipanga kuwashirikisha maafisa maendeleo ya jamii, maafisa ustawi wa jamii, Jeshi la polisi, watendaji Kata, mahakimu na pia waendesha mashtaka.
Bwire alisema kwamba, TAYOTA kama shirika binafsi wameguswa kuzijengea uwezo taasisi za kiserikali kwa kuwa wao ni wadau wenye wajibu wa kuisaidia Serikali katika kutekelezaji wa majukumu yake hasa ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
"Jukumu kubwa la kupambana na ukatili ni la Serikali, lakini mashirika yasiyo ya serikali ni wadau wa kuisaidia serikali kutekeleza majukumu yake hasa kupambana na ukatili, tunataka kuzijengea uwezo taasisi za kiserikali"alisema.
Kwa mujibu wa Bwire lengo kuu ni kutoa hamasa kwa serikali kupambana na ukatili hatua ambayo pia itasaidia kuhamasisha wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa mamlaka zinazohusika.
"Changamoto kubwa iliyopo visa vingi haviripotiwi kwa hiyo jamii inapaswa kupata uelewa, mara nyingi vitendo vya ukatili huathiri watoto kisaikolojia, wazazi wanapaswa kuelewa wao ndio wanajukunu la kumlinda mtoto"alisema Bwire.
Abubakari Killeo Kassim ni meneja miradi wa TAYOTA inayotekeleza mradi wa 'Pamoja tuwalinde', anasema lengo lao ni kutokomeza changamoto za ukatili wa kijinsia katika Jiji la Tanga.
Pia alisema, lengo la mradi huo uliyopo chini ya miradi ya Tanga yetu ni kuimarisha mifumo ya uwajibikaji baada ya kupokea changamoto za ukatili wa kijinsia na kwamba kata zote 27 zitahusishwa.
Alisema, mradi wa 'Pamoja tuwalinde' una maeneo makuu matatu, akitaja utoaji elimu kwa jamii juu ya suala zima la kuondosha ukatili, elimu ambayo itakuwa ikijumuisha sekta rasmi na isiyo rasmi.
Kwa sekta rasmi wataguswa vijana waliopo shuleni na kwenye taasisi mbalimbali huku sekta isiyo rasmi jamii nzima ikihusishwa huku wafanyakazi waliopo mstari wa mbele kupinga matukio ya ukatili kama jeshi la Polisi,maafisa maendeleo na maafisa wa kata wakijengwa.
Meneja mradi huyo alisema, watafanya uchechemuzi wa sera, kuboresha na kubainisha mapungufu yaliyopo ili kutoa mapendelezo juu ya namna ya kufanya maboresho kwenye maeneo yenye changamoto.
Naye Suleiman Msey kutoka kitengo cha elimu na hamasa amesema, dhamira iliyopo ni kuwafikia walengwa wengi popote walipo akiyataja maeneo ya shule na mitaani kutakakokuwa na program ya 'Kijiwe Salama cha Kahawa'.
"Miradi huu utafika maeneo mbalimbali kuanzia shuleni na mitaani, mtaani tutakuwa na program ya 'Kijiwe Salama cha Kahawa', hapa wanakusanyika watu wengi tutakuwa tukifanya mijadala" alisema Msey.
Msey alieleza kuwa Vijiwe hivyo vya Kahawa vitabaini changamoto na kuona namna ya kuziondosha kwa kushirikiana na wananchi husika katika wakati ambao Vijiwe hivyo vitageuzwa kuwa fursa kwa watu kupata elimu .
Pamoja na hayo Rehema Abdallah ambaye ni afisa kwenye mradi huo alisema, wanawake wanapaswa kutoa kipaumbele kushiriki vita dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, kwa maelezo kuwa jamii hiyo hususani wasichana chipukizi wamekuwa wenye kupitia changamoto nyingi katika umri wa ukuaji wao.
No comments