Breaking News

DKT. ASHA- ROSE MIGIRO MWANAMKE WA KWANZA KUWA KATIBU MKUU CCM

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Asha-Rose Migiro

................................................

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

Dkt. Asha-Rose Migiro ni mwanamke wa kwanza kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), nafasi ambayo haijawahiu kushikwa na mwanamke yeyote tangu Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961.

Nafasi hiyo ya Dkt. Migiro imekuja kufuatia uteuzi uliofanywa na Kikao cha Halmashuri Kuu ya CCM (Taifa) chini ya Mwenyekiti wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Migiro anashika nafasi hiyo ya juu katika chama hicho akimrithi Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye aliteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Dkt. Samia wa nafasi ya urais kupitia chama hicho.

Pamoja na kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM,Dkt. Migiro ana historia ya kipekee pia nchini kwani ni mwanamke wa kwanza kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa chini ya Katibu Mkuu wa umoja huo aliyestaafu Ban Ki-moon.

Kikao hicho pia kilimteua aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha  Kenani Kihongosi kuwa Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi  na Mafunzo wa chama hicho Taifa, akichukua nafasi ya Amos Makalla ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Dkt.Migiro alizaliwa mwaka 1956 na aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Alipewa cheo hicho na Katibu Mkuu wake Ban Ki-moon Januari 5, 2007

Hadi kuteuliwa kwa cheo cha Umoja wa Mataifa alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania tangu Januari 2006.

Nafasi hiyo alipewa na Rais Jakaya Kikwete aliyemteua kumfuata katika Wizara ya Mambo ya nje iliyoshikwa awali na Kikwete mwenyewe.

Chini ya Rais Benjamin Mkapa  Migiro alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Alikuwa Mbunge wa viti maalumu wanawake.

Kabla ya kujiunga na siasa alifundisha kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alisoma Shahada ya Awali na Shahada ya Uzamili katika chuo hichohicho.

Mwaka 1992 akaongeza Shahada ya Udaktari wa Sheria kwenye Chuo Kikuu cha Konstanz

 (Ujerumani). Akarudi Tanzania na kuanza kufundisha.

Dkt, Asha alifunga ndoa na Cleophas Migiro na kujaaliwa kupata watoto wawili wa kike.

Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Kenani Kihongosi

No comments