MWANGI ACHUKUA FOMU KUWANIA UDIWANI KATA YA IPEMBE MANISPAA YA SINGIDA
HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa
Singida imemteua kada wa chama hicho Omari Hamisi Mwangi kuwa mgombea wa
udiwani wa Kata ya Ipembe ambayo hiyo Manispaa ya Singida.
Mwangi leo Agosti 18, 2025 amekabidhiwa fomu ya kuwania
nafasi hiyo ambapo atapambana na wagombea wa vyama vingine kuwania nafasi hiyo
katika kata hiyo.
Katika kura za maoni zilizopigwa na wajumbe wa CCM wa kata hiyo
Mwangi aliibuka kidedea kwa kupata kura 86
dhidi ya Mohammed Ali ambaye alipata kura 34, Said Abdallah ambaye alipata kura
6 na Mwanahamisi Juma aliye ambulia kura 4.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu
hiyo alitaja baadhi ya vipaumbele vyake iwapo atashinda nafasi hiyo kuwa
atatenga ratiba ya kufanya mikutano na waananchi ili kujua changamoto zao ili
kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja.
“Nitafufua utaratibu wa kufanya mikutano ya mara kwa mara na
wananchi ili kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja na zile ambazo zitakuwa nje ya uwezo wangu
nitaziwasilisha ngazi ya juu kwa hatua ya utekelezaji,” alisema Mwangi huku
akishangiliwa na baadhi ya watu waliomsindikiza kuchukua fomu.
Alisema iwapo
atashinda katika kinyanganyiro hicho atahakikisha anashirikiana na wananchi wote
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuinadi ilani ya uchaguzi ya CCM
ya 2025/ 2030.
Wakati huo huo Mwangi amewataka wananchi na wana CCM kujitokeza
kwa wingi kushiriki kikamilifu kupiga kura katika Uchaguzi mkuu wa 2025 na kuhakikisha
wanawachagua wagombea wote wanaotokana na CCM Kuanzia Diwani, Mbunge na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt.
Samia Suluhu Hassan.
“Siku ya kupiga kura tukapige kura nyingi kwa wagombea wa CCM jambo ambalo litamsaidia Rais atakayetokana na CCM kufanya kazi yake kwa wepesi,” alisema Mwangi.
Mwangi mpaka anachaguliwa kuwa mgombea wa nafasi hiyo amekuwa akihudumu nafasi ya Katibu wa Hamasa wa CCM Kata ya Ipembe.
No comments