SKAUTI YAPONGEZWA KWA KUKABILIANA NA MAJANGA NCHINI
Mkurugenzi wa Operesheni Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Kanali Selestine Masalamedo akifungua mafunzo ya siku mbili ya elimu ya misaada ya kibinadamu kwa waratibu wa Skauti Tanzania yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Chuo cha Mipango Jijini Dodoma. Mafunzo hayo Mafunzo hayo yalisimamiwa na Mradi wa Kimataifa wa Skauti chini ya Shirika la Kimataifa la Skauti Duniani (WOSM)
...........................................
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
CHAMA cha Skauti Tanzania (TSA), kimepongezwa jinsi vijana wanavyojitokeza kwa wingi kukabiliana na majanga mbalimbali yanayotokea nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Operesheni Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Kanali Selestine Masalamado wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya elimu ya misaada ya kibinadamu kwa waratibu wa mikoa wa Skauti Tanzania yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Chuo cha Mipango Jijini Dodoma.
Kanali Masalamado alilishukuru Shirika la Kimataifa la Skauti Duniani (WOSM) kwa kufadhili mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwawezesha vijana na viongozi watu wazima kuchangia kikamilifu katika misaada ya kibinadamu, maandalizi ya kukabiliana na majanga na ujenzi wa ustahimililivu kwenye jamii.
“ Nitumie fursa hii kulishukuru WOSM kwa kuona kuna haja ya kuleta mafunzo haya Tanzania kwani ni wakati muafaka wa vijana kupata elimu hiyo ili kupata maarifa na ujuzi wa jinsi ya kukabiliana na majanga yanapojitokeza, akitolea mifano majanga yaliyotokea mkoani Manyara, kuzama kwa Kivuko cha Mwalimu Nyerere (Ukerewe), mafuriko ya Rufiji na kuanguka kwa ghorofa la Kariakoo, “ alisema Masalamado.
Alisema katika matukio hayo tuliona jinsi Skauti walivyokuwa mstari wa mbele katika kujitokeza kuokoa na kugawa misaada ya kibinadamu.
Alisema ni muhimu kuipitia Sera ya Taifa ya Maafa ili kujua muundo wake kuanzia ngazi ya Taifa mpaka kijiji / kitongoji ili kuimarisha mashirikiano katika ngazi hizo na kurahisisha ushiriki katika matukio mbalimbali yanapojitokeza.
Alisema milango ya ofisi yake ipo wazi kwa skauti wakati wowote kushirikiana mambo yanayohusu maafa.
Naye Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Abubakari Mtitu alilishukuru WOSM kuiamini Tanzania kuwa inaweza kutekeleza mradi huo ambao umetoa mafunzo hayo.
Aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha kuwa mafunzo waliyopata yanawafikia skauti wote waliochini yao na kwa hatua hiyo elimu hiyo itaenea kwa skauti wote na jamii yote nchini.
Alisema anajua siyo kazi rahisi lakini moyo wa kujitolea ndio unaohitajika zaidi.
Aidha, alishukuru mashirikiano mazuri yaliyopo kati ya Chama cha Skauti Tanzania na Ofisi ya Waziri Mkuu Manejimenti ya Maafa kwa kushirikishwa kwa kila jambo linalohusiana na maafa iwe matukio ya majanga, makongamano, mafunzo, maadhimisho na mengineyo na kuomba yaendelezwe.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu Msaidizi maafa na ubinadamu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mary Anyitike alilishukuru Shirika la Skauti Duniani kuwaletea mradi huo.
Alisema kupitia mafunzo hayo , idara za maafa katika ngazi zote za mikoa na wilaya zitaimarika na kufanya kazi kwa weledi tofauti na zilivyokuwa hapo mwanzo.
Aliishukuru pia Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa ushirikiano mkubwa wanaokipa Chama cha Skauti na kukitambua kuwa ni mdau mkubwa hasa katika shughuli za maafa yanapotokea.
Alisema bado wanahitaji msaada zaidi kutoka kwenye ofisi hiyo ili waweze kuwafikia skauti wote nchini na hivyo kusambaza elimu hiyo kwa jamii nzima na kupunguza athari kwa majanga mbalimbali yanapojitokeza.
Washiriki wa mafunzo hayo pia walipata mafunzo maalumu ya jinsi ya kujikinga na kutoa misaadambalimbali pale majanga ya moto yanapotokea kutoka kwa Jeshi la Zimamoto.
Mshiriki wa mafunzo hayo Ramadhani Ndasi kutoka Mkoa wa Kigoma alishukuru kupata fursa ya kupata mafunzo hayo ambayo yamewaongezea maarifa ya namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali nchini.
Mafunzo hayo yalisimamiwa na Mradi wa Kimataifa wa Skauti chini ya Shirika la Kimataifa la Skauti Duniani (WOSM)
Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Abubakari Mtitu, akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Kamishna Mkuu Msaidizi maafa na ubinadamu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mary Anyitike akitoa shukurani kwa wawezeshaji wa mafunzo hayo.
Maafisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakitoa mafunzo ya namna ya uokozi wakati wa majanga
Afisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji akifundisha namna ya kumbeba mtu wakati wa uokoaji.
Mafunzo zaidi yakitolewa na maafisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Mshauri wa Maafa na Ubinadamu kutoka WOSM, Devina Adosi akielekeza jambo wakati alipokuwa akitoa mada.
No comments