Breaking News

ANGELO MADUNDO ANAVYOING’ARISHA JUMUIYA YA WAZAZI CCM MBINGA

Atamba kupata ushindi mnono uchaguzi mkuu

Ajivunia mambo matatu

Awaomba wananchi na wana CCM kujitokeza kwa wingi kumlaki Dkt. Samia ambaye atawasili Septemba 21, 2025 Mkoa wa Ruvuma.

 Mratibu wa timu ya kampeni za Mgombea Ubunge Jimbo la Mbinga Vijijini Angelo Madundo, akimnadi Mgombea huyo Wakili Judith Kapinga kwenye moja ya mikutano ya kampeni inayoendelea kwa kasi jimboni humo.

................................. 

Na Dotto Mwaibale

UMOJA wa Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliundwa mwaka 1955 ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuundwa kwa chama cha TANU mwaka 1954.

Umoja huu uliundwa ukiwa na misingi mikuu miwili, Elimu pamoja na Malezi, na mtu mwenye umri usiopungua miaka 18 anaweza kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo.

Majukumu ya jumuiya ya wazazi ni kuhamasisha wazazi na watanzania wa rika zote juu ya umuhimu wa elimu pamoja na kuanzisha na kusimamia shule za jumuiya .

Jukumu lingine ni kusimamia maadili na malezi bora kwa vijana na jamii kwa ujumla ili kujenga taifa lenye maadili na linalosimamia misingi ya utamaduni wa Tanzania.

Pia kusimamia rasilimali pamoja na shughuli za kiuchumi zilizopo na kubuni miradi mipya, kwa manufaa ya Jumuiya na Taifa kwa ujumla.

Malengo ya jumuiya ya wazazi ni kuhakikisha kuwa, wazazi kama nguzo ya jamii wanashiriki katika ustawi wa chama na taifa kwa kusimamia elimu, malezi na maadili kwa faida ya kizazi  hiki na vizazi vijavyo na kuhakikisha chama cha mapinduzi kinakua imara katika nyanja zote.

Jumuiya wazazi wa CCM ndiyo jumuiya mama kati ya jumuiya zote kwa maana nyingine tunaweza kusema ndiyo injini ya chama.

Viongozi wa Jumuiya hiyo kuanzia Mwenyekiti wake, Katibu Mkuu wa Taifa, Mkoa, Wilaya hadi  kata tumeona namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana na jumuiya nyingine za chama hicho katika kutekeleza majukumu ya kazi ya kila siku.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Taifa, Ally Hapi tumekuwa tukimuona jinsi ambavyo hapati hata muda wa kupumzika ili kuhakikisha shughuli mbalimbali ndani ya jumuiya hiyo zinakwenda sawa.

Hali hiyo imekuwa ikiigwa na watendaji  wa jumuiya hiyo nchini jambo ambalo ni zuri katika ustawi wa CCM kupitia jumuiya zake zote.

Jumuiya hizo ni Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu na idara ya Chipukizi ambayo inaanzia chini kabisa kuwaandaa watoto katika malezi na maadili.

Nimeanza kuandika Makala hii kwa kuelezea majukumu na umuhimu wa Jumuiya hii ya wazazi ni kutokana na kuwapika viongozi wake katika utekelezaji wa majukumu yake, leo napenda kumzungumzia Angelo Madundo ambaye ni Katibu wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Madundo amekuwa akifanya kazi zake bila ya kuchoka wakati wowote unapompigia simu kwa ajili ya kazi simu yake inapokelewa kwa wakati na kukusikiliza.

Jambo hilo linaleta matumaini kwa wananchi ambao wanahitaji kupata huduma mbalimbali kupitia kwa viongozi wa jumuiya kubwa kama hiyo ndani ya CCM.

Madundo tumemuona jinsi ambavyo anashirikiana na jumuiya za chama hicho na viongozi wa chama hicho katika wilaya hiyo wakati wa utekelezaji wa majukumu yake ya  kazi jambo ambalo linaleta afya ya maendeleo katika wilaya hiyo.

Hatua hiyo, inaonesha mshikamano wa dhati ambao unaunga mkono moja kwa moja jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea wananchi maendeleo kutokana na uwajibikaji wenye tija kwa taifa.

Hivi sasa Taifa letu lipo kwenye kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika oktoba 29, 2025 ambapo tutamchagua rais, wabunge na madiwani ambapo chama kitakachopata ushindi kitaingia kushika dola.

Kwa Jimbo la Mbinga Vijijini ambalo mgombea nafasi ya ubunge kupitia CCM ni Wakili Judith Kapinga (Maarufu kama Malikia wa Mbinga), wao wameunda kamati maalum ya ushindi huku Madundo akiwa ni Mratibu wa timu ya kampeni na Mwenyekiti wa kampeni hizo akiwa ni John Bosco Mkandawile.

Kupitia kamati hiyo tumeona kasi ya kampeni zinazofanyika katika jimbo ambapo kwa siku moja wanafanya kampeni katika kata zaidi ya tatu na vijiji sita huku mikutano yao ikijaza watu kutokana na kuiandaa vizuri.

Katika mikutano hiyo tumeona jinsi mgombea nafasi ya ubunge anavyo tangaza sera na kuinadi ilani ya chama hicho na kumuombea kura mgombea wa urais, diwani na yeye mwenyewe huku akihimiza oktoba 29 wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM.

Katika maeneo mengine ya mikutano hiyo viongozi wa kamati hiyo wamekuwa wakimnadi mgombea huyo wa nafasi ya ubunge na kumuombea kura rais, mbunge na diwani wa kata husika.

Madundo anasema kujiandisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ni jambo moja lakini jambo ambalo ni kubwa na la msingi ni siku ya kupiga kula wananchi wote na wana CCM wajitokeze kwenda kupiga kura

Ushirikiano wa namna hiyo unaonesha mafanikio ya mapema ya ushindi wa chama hicho kutokana na jinsi walivyojipanga.

Madundo anasema tangu aanze kufanya kazi katika wilaya hiyo zaidi ya miaka mitano anajivunia mambo makubwa matatu la kwanza likiwa ni kuifufua Shule ya Sekondari ya Mkinga ambayo ni ya Jumuiya ya Wazazi ambayo aliikuta ipo taabani.

Aliongeza kuwa utokana na hali hiyo alitoa taarifa makao makuu ambao walimpa baraka zote za kuinusuru shule hiyo ili ili irudi katika hali yake ya kawaida.

Madundo anasema shule hiyo aliikuta ikiwa na wanafunzi 120 haina jengo la utawala, madarasa machache ambapo alitengeneza mpango kwa ajili ya kuwapata wadau wa maendeleo ili kusaidia jambo hilo.

Anasema wadau wa kwanza walikuwa ni viongozi wa chama na Serikali ambao kwa umoja wao walifanikisha kujenga jengo kubwa la kisasa la utawala.

Anasema kazi nyingine aliyoifanya katika shule hiyo alianzisha kidato cha tano na cha sita kwa lengo la kuongeza idadi ya wanafunzi na huduma ya masomo ya juu kwa wanafunzi hao hatua ambayo imeongeza wanafunzi kutoka 120 mwaka 2020 hadi kufikia zaidi ya 351.

“ Katika rekodi za kitaaluma shule yetu imekuwa ya kwanza kwa kuongoza matokeo kiwilaya lakini kimkoa mara kwa mara imekuwa ishishika nafasi ya kumi bora,” alisema Madundo.

Anasema katika eneo hilo la elimu anashukuru Mungu na Serikali kwani wamepiga hatua nzuri na wanatarajia kufanya vizuri zaidi siku za mbele kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina yao na wadau wa maendeleo.

Madundo anasema jambo la pili ambalo anajivunia ni ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Wilaya ambayo ipo Mbinga Mjini na kazi hiyo ilifanikiwa baada ya kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo.

“Kutokana na kazi hizo kikao cha kamati ya utekelezaji Mkoa wa Ruvuma kilinitunuku barua ya kunipongeza jambo ambalo nashukuru sana,” alisema Madundo.

Anasema mafanikio ya tatu ameanzisha mradi wa duka la kisasa la makaa yam awe ambao upo katika hatua za majaribio na jingo lake limekwisha kamilika.

Anasema isingekuwa suala la uchaguzi wangekuwa wameuzindua chini ya kauli mbiu yao ya ‘Uchumi na Siasa’ aliyoianzisha.

Madundo anasema kuwa lengo la kuanzisha mradi huo ni kulenga viongozi wa kisiasa kupitia jumuiya zao kuhamasika kuwa na miradi ya kuwaongezea kipato.

Anasema kupitia mradi huo wameingia ubia na Kampuni ya Jitegemee ambayo ni ya CCM kwa ajili ya kuchukua bidhaa ya kupikia na kuisambaza kwenye shule mbalimbali, mahotelini na maeneo mengine yanayotumia nishati hiyo kwa matumizi ya kupikia.

Anasema kwa wakala waliopewa watakuwa wasambaji wakuu wa nishati hiyo kwa mkoa mzima wa Ruvuma.

“Nshukuru kwa kipindi hiki ambacho nikiwa kama kiongozi, jumiya yetu imebadilika ndani ya Wilaya ya Mbinga na mkoa kwa ujumla kwa kuitambulisha kwa mambo tofauti kwenye maeneo ya ziara za kimkakati za kuimarisha chama,” alisema Madundo.

Madundo anasema ushirikiano mkubwa na jumuiya za chama hicho na idara za Serikali mkoani hapo ndiyo siri kubwa ya mafanikiyo yao.

Akizungumzia kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu anasema malengo ya Jimbo la Mbinga Vijijini ni kuongoza kwa kra za rais kitaifa na kwa takwimu za kwetu mgombea wetu wa nafasi ya ubunge Judith Kapinga aliongoza kwa kupata kura nyingi zaidi ya 12,000 kitaifa za kura za maoni.

“Malengo yetu ni kuongoza kitaifa kwa kura zote kuanzia za rais, mbunge na madiwani,” aliseam madundo.

Madundo aliongeza kuwa mikutano yao yote wanayoifanya imekuwa na mafanikio makubwa kwani chini yake imeratibiwa vizuri kisayansi na ina jaza watu.

Alisema hali hiyo ni ishara tosha ya kupata kura nyingi kutokana na wananchi kukielewa chama na sera zake na zaidi wagombea wao ni wazuri kuanzia rais, mbunge na madiwani hivyo wanarajia kuwa ndani ya majimbo matano bora nchi nzima yakatakayofanya vizuri kwa kupata kura nyingi.

Aidha, Madundo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wana Mbinga kujitokeza kwa wingi kumpokea Mgombea wa nafasi ya Urais wa CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajia kuwasili mkoani Ruvuma siku ya Jumapili Septemba 21, 2025.

Mratibu wa timu ya kampeni za Mgombea Ubunge Jimbo la Mbinga Vijijini Angelo Madundo, akimkabidhi ilani ya uchaguzi mgombea huyo wakili Judith Kapinga kwenye moja ya mikutano ya kampeni inayoendelea imboni humo.
Jengo la Utawala la Mkinga High School.
Jengo la mradi wa duka la Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mbinga. Kwa ajili ya kuuza nishati mbadala ya kupikia ya makaa ya mawe.

Ukaguzi wa ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mbinga ambayo ujenzi wake unaendelea chini ya katibu wa jumuiya hiyo, Angelo Madundo (kushoto kwenye picha).

No comments