Breaking News

BURIANI ABBAS MWINYI MWENDO UMEUMALIZA KAPUMZIKE KWA AMANI

Abbas Ali Mwinyi enzi za uhai wake

..............................

Na Dotto Mwaibale

MAMIA ya waombolezaji walijitokeza kwa wingi kumzika Abbas Mwinyi, mtoto wa aliyekuwa Rais mstaafu wa Zanzibar, Hayati Ali Hassan Mwinyi, na kaka wa Mgombea Urais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Abbas alifariki usiku wa kuamkia Septemba 25, 2025 katika Hospitali ya Mkoa wa Lumumba na mazishi yake kufanyika Septemba 26 katika makaburi ya familia Mangapwani.

Viongozi mbalimbali wakiwepo wa dini wananchi ndugu, jamaa na marafiki walihudhuria mazishi yake huku mitaa ya Unguja ikikugubikwa na huzuni wakati jeneza lilipobeba mwili wake likiwa limebebwa kutoka Msikiti wa Zinjibar.

Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaab, ndiye aliyewaongoza waumini kwenye sala ya jeneza. Kisha, kwa heshima ya kitaifa, Mufti Mkuu wa Tanzania, Dk Abubakar Zubeir, aliongoza sala ya mazishi Mangapwani.

Wananchi walimwelezea Abbas kuwa alikuwa ni mtu mpole, mnyenyekevu, asiye na majivuno licha ya hadhi ya familia yake huku baadhi yao wakisema  hakutumia jina la baba yake wala nafasi ya mdogo wake kama ngao ya majivuno, bali alijijengea heshima yake kwa unyenyekevu na upendo kwa watu.

Abbas ambaye alikuwa ni rubani mstaafu aliingia kwenye siasa mwaka 2020 na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Fuoni na kupitia nafasi yake hiyo aliwatumikia wananchi kwa weledi mkubwa.

Abbas ndugu yetu mwendo umeumaliza kapumzike kwa Amani utakumbukwa kwa mengi.

Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Abbas Mwinyi wakati wa mazishi yake 
Mazishi ya Abbas Mwinyi yakifanyika
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akimpa pole Mjane wa Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi kufuatia msiba huo. 

No comments