Breaking News

DC ILALA ATAKA HAKI UTATUZI MIGOGORO MABARAZA YA KATA

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akizungumza  wakati wa mafunzo na hafla ya kuwaapisha wajumbe wa mabaraza  ya kata wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliyofanyika Septemba 26, 2025 katika Ukumbi wa Shule ya Msingi Kisutu Jijini Dar es salaam. 

................................

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wajumbe wa mabaraza ya kata wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kutenda haki wakati wa usuluhishi wa migogoro katika kata zao. 

Mpogolo aliyazungumza hayo Septemba 26, 2025 wakati wa mafunzo na hafla ya kuwaapisha wajumbe wa mabaraza hayo Jijini Dar es salaam. 

Alisema watu wanaweza kuzani kazi hiyo wanayoenda kuifanya ni ndogo,  kazi ya usuluhishi ambayo haina kipato ni kazi kubwa sana ni kazi ambayo wanakwenda kubeba lawama. 

Alisema hata baba na mama kusuluhisha watoto wao tu ndani ya familia kuna kuwa na changamoto kubwa kwani ni kazi ambayo kila mwanadamu anaamini ndiyo kazi inayojenga umoja na mshikamano miongoni mwao. 

“Ninyi mmeteuliwa miongoni mwa wahitaji wengi hivyo mnapaswa kwenda kutenda haki wakati wa utatuzi wa migogoro,” alisema Mpogolo. 

Alisema wilaya ya Ilala ina wakazi wasiopungua milioni moja na laki sita ni watu wengi na kila mtu ana mgogoro na kwenye jamii ya watu wa ilala yenye idadi nyingine ya watu hao wanaingia ndani ya  wilaya hiyo kwa ajili ya kufanya biashara na wanaotegemewa kutuliza migogoro yao ni wajumbe hao. 

“ Nina kila sababu ya kuwashukuru na kuwapongezeni sana kwa kazi hiyo kubwa mnayoifanya ya usuluhishi,” alisema Mpogolo huku akipigiwa makofi. 

Alisema katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria ya mabaraza wajumbe hao ndiyo wasuluhishi ambao wanabeba mahusiano makubwa zaidi kuliko hukumu. 

Mpogolo aliongeza kuwa usuluhishi ni pande zote mbili zinaafikiana nini kifanyike na hukumu msimamizi ndiye anayehamua nani apate haki na nani hakose,  lakini wao ni vyombo vya wananchi kwa ajili ya kuwasaidia wapate amani, utulivu na mshikamano wao na ndiyo maana imetengenezwa suluhu. 

“Suluhu hii ya upatanishi haijaishia kwenye katiba tu peke yake bali ipo hata kwenye vitabu vya dini zote mbili waislam na wakristo  ambapo katika kuraan surah Al-Baqara (2:224) ina sema Mwenyezi Mungu ni msamehevu, mpole, Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaofanya suluhu,” Mpogolo alinukuu sura hiyo katika kuraani tukufu. 

Kwa upande wa wakristo Mpogolo  alisema katika Mathayo 5:9 inasema “ Heri ya wapatanishi kwa maana hao wataitwa wana wa Mungu,”. 

Mpogolo aliwaambia wajumbe hao kuwa maneno hayo yote ya Mungu yanaelekeza kwenye usuluhishi hivyo wanatakiwa kwenda kutenda haki kwa watu wanaotakiwa kupata haki zao na suluhu. 

Alisema misingi itakayopatikana wakati wa kutafuta haki hizo ndiyo itakayotumika katika hatua nyingine za juu kama sehemu ya rejea. 

Alisema kuna watu wengi wanabubujikwa na machozi kutokana na hatua za ujanja ujanja zinazofanywa bila ya kuzingatia haki na kuwa wao ndiyo msingi wa maamuzi ya mahakama hivyo ambapo aliwata waende wakafanya kazi hiyo kwa haki. 

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala Bi. Charagwa Sulemani amewataka wajumbe hao, kuwa wavumilivu na kutatua changamoto kwa hekima uadilifu katika kufanya suluhu kwa wananchi katika maeneo yao. 

Katika hafla hiyo jumla ya wajumbe 288 kutoka kata 36 za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam waliapishwa  na kula kiapo cha uadilifu. 

Wajumbe hao wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba, sheria na kanuni zinazoongoza uendeshaji wa Serikali za Mitaa. 

Mabaraza ya Kata ni vyombo vilivyoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha sheria ya mabaraza ya kata ya mwaka 1985, ambapo kila baraza linajumuisha wajumbe wasiopungua wanne na wasiozidi wanane watakaochaguliwa na kamati ya kata kutoka miongoni mwa majina ya wakazi wa kata yaliorodheshwa kwa kuzingatia utaratibu maalum uliowekwa.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo akizungumza na wajumbe hao.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, akiwa na viongozi wengine meza kuu wakiimba wimbo wa Taifa.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi. Charagwa Sulemani, akisisitiza jambo kwa wajumbe hao.
Wajumbe hao wakiwa kwenye hafla hiyo.
Taswira ya hafla hiyo.
Wajumbe wakiwa kwenye hafla hiyo
Hafla ikiendelea.
Wajumbe wakiwa kwenye hafla hiyo.
 

No comments