KAMPUNI ZA DNATA, EMIRATES LEISURE RETAIL ZANZIBAR ZAFANYA USAFI UFUKWENI
Wafanyakazi wa Kampuni za Dnata na Emirates Leisure Retail Zanzibar wakifanya usafi wa mazingira katika Ufukwe wa Buyu uliopo Chukwani Zanzibar Septemba 18, 2025.
......................................
Na Dotto Mwaibale, Zanzibar
KAMPUNI za Dnata na
Emirates Leisure Retail Zanzibar zimeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi za utunzaji wa mazingira kwa kufanya usafi wa Ufukwe wa
Buyu uliopo Chukwani.
Katika muendelezo wa kuungamkono jitihada hizo za Serikali
za uhifadhi na utunzaji wa mazingira leo Septemba 18, 2025 kampuni hizo
zimeshirikiana kufanya kazi hiyo katika ufukwe huo.
Afisa Utawala Msaidizi wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail
Zanzibar, Ramadhan Hussein Layya (Maarufu Msokolo), akizungumza na waandishi wa
habari alisema kampuni hizo zimekuwa na utaratibu wa kushirikiana katika mambo
mengi likiwemo la kufanya usafi.
“Kazi hii ya utunzaji wa mazingira kwa kufanya usafi
makampuni yetu yamekuwa yakishirikiana na kwetu jambo la utunzaji wa mazingira
ni endelevu na siyo la Serikali pekee ndiyo maana tunaiunga mkono,” alisema
Msokolo.
Alisema zoezi hilo la kufanya usafi halikulenga kuondoa
takataka tu katika ufukwe huo, bali kuchukua jukumu la kulinda mazingira,
kuhifadhi viumbe wa baharini, na kuhakikisha urembo wa asili wa Zanzibar
unabaki salama kwa vizazi vijavyo.
Msokolo alisema zaidi ya wafanyakazi 50 kutoka katika
kampuni hizo walishiriki katika kazi hiyo ya kufanya usafi ambapo waliweza
kukusanya kilo 1,000 za chupa za plastiki na taka mbalimbali kutoka ufukweni na
chini ya bahari.
“ Kila chupa iliyokusanywa kwetu imekuwa ni hatua moja ya
kusonga mbele kuelekea bahari safi na sayari yenye afya,” alisema Msokolo.
Alisema hatua hiyo kwao ni ushuhuda kuwa mshikamano na
bidii vikijumuika, wanaweza kufanya mabadiliko makubwa ya utunzaji na uhifadhi
wa mazingira.
Msokolo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wote waliojitokeza kushiriki
katika kazi hiyo na kusisitiza kuwa umoja siku zote ni nguvu na kujitoa kwao kuna
maana kubwa katika utunzaji wa mazingira chini ya kauli mbiu yao “Tuwe pamoja kulinda fukwe, bahari na
mazingira yetu — hatua moja baada ya nyingine”.
Katika kazi hiyo viongozi wa kampuni hizo walishiriki akiwepo Meneja Mkazi wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail, Paul Atallah na Meneja Mkazi wa Kampuni ya DNATA, Maruan Essa ambao kwa pamoja walijumuika na wafanyakazi wao kufanikisha shughuli hiyo na kuonesha mfano bora wa viongozi wanaojitoa kwenye shughuli za kijamii.
Usafi ukiendelea kufanyika.Wafanyakazi hao wakiwa na viroba vyenye takataka baada ya kufanya usafi kwenye ufukwe huo.
Usafi ukifanyika.
Kazi ya usafi ikiendelea
Usafi ukifanyika
Afisa Utawala Msaidizi wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail Zanzibar, Hussein Ramadhani Layya (Maarufu Msokolo), akiwa amejitwisha kiriba chenye takataka wakati wa ufanyaji huo wa usafi.
Wafanyakazi wa kampuni hizo hizo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufanya kazi hiyo ya usafi
Wafanyakazi wa kampuni hizo hizo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufanya kazi hiyo ya usafi
No comments