TBS YAZINDUA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 TANGU KUANZISHWA
Viongozi mbalimbali wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),wakishiriki uzinduzi rasmi wa Maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 1975. Mgeni rasmi alikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil T. Abdallah.
...............................
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limezindua rasmi Maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975 ambapo tukio hilo lililohudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil T. Abdallah.
Akizungumza katika Maadhimisho hayo ambayo yamefanyika Septemba 18, 2025 katika ofisi za TBS zilizopo Ubungo Jijini Dar es Salaam ambapo Dkt. Abdallah amesema shirika hilo linafanya kazi kubwa ya kuhakikisha viwango vya ubora wa bidhaa unafikiwa.
Aidha amesema kuwa Shirika limeendelea kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi na wadau kutokana na kuboreshwa kwa mifumo ya kielektroniki na uimarishaji wa ofisi za kanda.
"Mwezi Juni, 2025 tumeshuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa maabara mpya na ya kisasa Kanda ya kati Dodoma ambapo ujenzi umefikia asilimia 86, kuendelea kwa Mradi wa ujenzi wa Maabara na Ofisi Jijini Mwanza ambao umefikia asilimia 48 na kukamilika kwa usanifu wa Mradi wa ujenzi wa Maabara na Ofisi jijini Arusha". Amesema
Amesema kuwa hatua hizo zitasaidia wananchi na wadau wa Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini na maeneo ya mikoa jirani na kanda hizi kupata huduma kwa haraka na kwa gharama nafuu.
Amesema kaulimbiu ya maadhimisho hayo yanayotarajia kuhitimishwa desemba mwaka huu, yana kaulimbiu ya "Uhamasishaji Ubora na Usalama kwa Maisha Bora" ambayo itasaidia kuendelea kujenga uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uzingatiwaji wa viwango vya ubora na uimarishwaji wa bidhaa na huduma za viwango.
Amesema katika kipindi cha miaka 50, TBS imepiga hatua kubwa ikiwe kupanua wigo wa utoaji huduma na kuzisogeza kwa wananchi pamoja na kuboresha mifumo ya kielektroniki.
"Katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, TBS imejenga heshima kubwa kimataifa kutokana na utekelezaji mahiri wa majukumu yake kwa kupata tuzo mbalimbali ikiwepo ya Mdhibiti Bora Barani Afrika na kupata daraja la juu la Shirika la Afya Duniani (WHO), kuwa wa kwanza SADC kupata Ithibati ya Kimataifa ya uthibitishaji ubora, na ilifanikiwa kupata Ithibati ya kimataifa ya mfumo wa usimamizi wa chakula" amesema Dkt. Abdallah.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Ashura Katunzi, ameeleza safari ndefu ya mafanikio ya Taasisi hiyo katika kipindi cha nusu karne, ikiwemo kuandaa zaidi ya maelfu ya viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa vilevile amebainisha kuwa hatua hizo zimeiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa Nchi kinara katika eneo la viwango barani Afrika.
Dkt. Katunzi amesema TBS imefanikiwa kuandaa viwango katika sekta mbalimbali kwa kushirikisha wadau husika.
Amesema vyeti na leseni za ubora vimetolewa kwa wazalishaji zaidi ya 4000 wakiwemo wajasiriamali wadogo zaidi ya1700 ambao hupata huduma hizo kwa ufadhili wa Serikali, hatua ambayo imewawezesha wazalishaji kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi makatakwa ya masoko ya ndani na kimataifa.
Amesema Shirika lina jumla ya maabara 12 zenye ithibati ya umahiri kimataifa, jambo linalowawezesha wadau kupata matokeo yanayokubalika kimataifa hivyo kurahisisha biashara za kimataifa.
"Maabara hizi zinavifaa vya kisasa na vya kipekee barani Afrika ambapo ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi kwani hutoa matokeo sahihi yanayotambulika na kuaminika ulimwenguni kote". Amesema
Wakati wa kuelekea kwenye maadhimisho hayo, ambayo yatafanyika Mwezi Desemba katika ukumbi wa Mlimani City, inatarajia pamoja na mambo mengine kutakuwa na matukio mbalimbali kama Viwango Marathon na Viwango Business Forum na sherehe za kilele cha maadhimisho hayo.
Maadhimisho haya yatawakutanisha wadau zaidi ya mia tano (500) wa masuala ya ubora, viwango, viwanda na biashara kutoka ndani na nje ya nchi kujadili kwa pamoja na kutafuta suluhu ya changamoto za masuala ya viwango, uzinduzi wa Kitabu cha historia ya TBS na maonesho ya Biashara kutoka katika taasisi za Umma na Binafsi.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasema “Uhamasishaji wa Ubora na Usalama kwa Maisha Bora.” Viongozi hao wametoa wito kwa Watanzania wote kushirikiana na TBS ili kuhakikisha viwango vinakuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Ashura Katunzi, akizungumza kwenye uzinduzi huo.Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil T. Abdallah, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Uzinduzi ukiendelea. Kutoka kulia ni Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi TBS, Bw. Sufiani Hussein Ally, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil T. Abdallah. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Ashura Katunzi na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Sempeho Manongi
Uzinduzi ukiendeleaUzinduzi ukiendelea
Viongozi wakiwa kwenye uzinduzi huo, Kutoka kulia ni Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi na Mjumbe wa bodi ya Wakurugenzi TBS, Bw, Sufiani Hussein Ally, Bi. Solana Msimbe mfanyakazi mstaafu wa TBS, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil T. Abdallah. Mfanyakazi mstaafu wa TBS Aloyce Nshange na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Ashura Katunzi.
No comments