Breaking News

KANISA LA ABC, TABATA JIJINI DAR ES SALAAM LAENDELEA KUWAKUMBUKA WAHITAJI

Askofu Mkuu wa Kanisa la Abundant Blessing Church (ABC), Flaston Ndabila akizungumza na wahitaji katika hafla ya kuwakabidhi mahitaji mbalimbali iliyofanyika Desemba 27, 2025 Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mandela Tabata, Leonard Chalema.

......................................

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam 

KANISA la Abundant Blessing Church (ABC), lenye makao yake makuu  Tabata Mtaa wa Mandela jijini Dar es Salaam limeendelea kusaidia watu wenye uhitaji, wajane, wagane na watoto yatima ili nao wafurahie sikukuu za mwishoni mwa mwaka. 

Kanisa hilo kupitia Askofu wake Mkuu Flaston Ndabila kila mwaka limekuwa likitoa msaada wa vyakula, sukari, nguo na mafuta ya kula kwa watu wenye uhitaji wanaoishi jirani na kanisa hilo pamoja na vifaa vya shule kwa watoto wasiyokuwa na uwezo.

 Akizungumza Desemba 27, 2025 wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mahitaji mbalimbali kwa watu wenye uhitaji Askofu Ndabila alisema wanajisikia furaha kujumuika na wahitaji kwa kuwapa baadhi ya mahitaji yao.

Alisema lengo kuu la kufanya hivyo si kuonesha wanavyofanya bali ni kuhamasisha jamii kujenga tabia ya kuwakumbuka wahitaji kwa kuwapa misaada mbalimbali kama neno la Mungu linavyofundisha.

Alisema msaada huo umewezeshwa na watu mbalimbali wakiwemo waumini wa kanisa hilo na kazi ya kanisa hilo ni kuratibu ukusanyaji wa vitu hivyo na kuwakabidhi walengwa.

“Yanapotokea matukio ya dharura kama vile mafuriko tumekuwa tukiwatembea wahanga na kuwasaidia  na tunafanya hivi ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali yetu inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wenye uhitaji ili kuwapa faraja,” alisema Ndabila. 

Askofu Ndabila alisema sasa ni takribani miaka 15 kanisa hilo limekuwa likifanya ibada hiyo ya kuwakumbuka wahitaji ambapo wahitaji zaidi ya 50 kila mwaka wamekuwa wakisaidiwa.

Mkazi wa eneo hilo Mzee Michael Hodi akizungumza kwa niaba ya wenzake aliushukuru uongozi wa kanisa hilo kwa kuwakumbuka wahitaji kila mwaka kwa kuwapatia msaada na kuomba taasisi zingine za dini na zisizo za kiserikali kujitokeza kuwasaidia.

Aidha, Mzee Hodi aliipongeza Serikali kwa kuimarisha amani baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025 na kuwaomba watanzania kuungana na serikali katika kudumisha amani kwani inapokosekana wahanga wakubwa ni watu wenye uhitaji, watoto na wanawake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mandela Tabata, Leonard Chalema, alimshukuru Askofu Ndabila kwa msaada anaoutoa kila mwaka kwa wahitaji wa mtaa huo na kueleza kuwa Serikali ya mtaa huo inautambua mchango wa kanisa hilo kwa jamii na itaendelea kushirikiana nalo.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Abundant Blessing Church (ABC), Flaston Ndabila akizungumza na wazee wahitaji.

Mke wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Abundant Blessing Church (ABC), Janeth  Ndabila akizungumza na wahitaji (hawapo pichani).

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mandela Tabata, Leonard Chalema, akizungumza katika hafla hiyo.

Mzee Michael Hodi akitoa shukurani kwa uongozi wa kanisa hilo kwa niaba ya wenzake

Mjumbe wa Serikali ya mtaa huo akishukru kwa msaada huo.
Wajane wakiwa kwenye hafla hiyo.
Muonekano wa mifuko yenye unga waliokabidhiwa wahitaji hao.
Wafanyakazi wa kanisa hilo wakiwa kwenye hafla hiyo.
Mmoja wa wazee akikabidhiwa nguo.
Askofu Flaston Ndabila akimkabidhi kiroba cha unga Mzee Hussein Kibalanga.
Mke wa Askofu Flaston Ndabila akimkabidhi nguo mmoja wa wazee wa mtaa huo.
Mzee Michael Hodi akikabidhiwa kiroba cha unga.
Askofu Ndabila akimkabidhi mfuko wa sukari, unga na nguo mmja wa wazee wa mtaa huo.
 

No comments