Breaking News

DAWA, VIFAA TIBA VISIVYO NA UBORA HATUVITAKI SINGIDA

Katibu Tawala Msaidizi wa Huduma za Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Singida, Stanslaus Choaji ambaye alikuwa mgeni rasmi akifungua mafunzo hayo.

...........................

Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)

MKOA wa Singida hautakuwa tayari kuwa dampo la matumizi ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambavyo havina havina ubora.

Katibu Tawala Msaidizi wa Huduma za Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Singida, Stanslaus Choaji aliyasema hayo Machi 12, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wataalamu, wakaguzi na wafamasia wa Halmashauri za wilaya ambao wanakagua dawa, vifaa tiba na vitendanishi yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA)

 Choaji alisema jukumu la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya na kuweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa Taifa.

"Hilo ni jukumu kubwa la Serikali na mtaona jinsi inavyofanya kila jitihada kadili itakavyowezekana kwa kutumia rasilimali mbalimbali ili kuwawezesha na kuona wananchi wanapata huduma bora za afya," alisema Choaji.

Alisema kutokana na jitihada hizo zinazofanywa na Serikali wakaguzi hao na watendaji kwenye eneo lao wanaweza kuonesha jinsi ambavyo wanashiriki kwenye hizo jitihada za Serikali kwa kutekeleza majukumu hayo kama vile inavyotakiwa.

Choaji alisema majukumu ya wataalamu hao ni ya msingi kwa sababu yanahusisha maisha ya binadamu hivyo kutekeleza jukumu hilo la kusaidia binadamu ni  kutekeleza jukumu la Mungu aliye tuumba.

Alisema kutenda tofauti na majukumu hayo na kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyotumika na binadamu ni kwenda kinyume kabisa na kusudio la Mungu la kumuumba binadamu na mifugo ambayo nayo ni viumbe hai.

Aliwaomba kufanya kaguzi zao kwa kuzingatia kanuni na maadili kwa lengo la kulinda afya za jamii  na kuwahakikishi uwepo wa bidhaa salama

"Tusingependa sisi Mkoa wa Singida tuwe na changamoto ya matumizi ya vifaa hivyo ambavyo havina sifa," alisema Choaji.

Kwa upande wake Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa alisema kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanalinda afya ya jamii kwa kuhakikisha bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi ni bora salama na zenye ufanisi.

Alisema ili jukumu hilo liweze kutekelezeka kwa kuzingatia ukubwa na upana wa nchi yetu yenye halmashauri za wilaya na   mikoa mingi takribani 26 kwa upande wa Tanzania Bara TDMA kwa kuzingatia uchache wa watumishi wake waliona haitakuwa rahisi kufika kila kona ya nchi ndipo kanuni ya kukasimu baadhi ya majukumu na madaraka ya TMDA iliandaliwa na kupitishwa ili majukumu hayo yaweze kukasimiwa kwa halmashauri za wilaya.

Alisema majukumu hayo yamepelekwa katika halmashauri  hizo ili ziweze kusaidia kufanya baadhi ya majukumu ya TMDA kwa kufanya ukaguzi na kuhakikisha wanafuatilia bidhaa ziwe bora na salama katika soko pia kufanya usajili wa maeneo ya kutolea huduma ambayo yapo chini ya TMDA.

"Leo tumewaalika wakaguzi kutoka halmashauri saba za Mkoa wa Singida tumejumuika kwa pamoja ili tuweze kupeana ABC jinsi ya kufanya kazi hizo ambazo zimekasimiwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa tupo hapa na wataalamu wakaguzi wa  mifugo, wafamasia, wataalamu wa maabara na dawa na wote hawa wanahusika kwa namna moja ama nyingine kuhakikisha hizo bidhaa zinawafikia walengwa ambao ni wananchi.

Washiriki wa mafunzo hayo Upendo Kiula ambaye ni Mratibu wa Huduma za Maabara kutoka Wilaya ya Itigi na Alfred Rwamtoga Mfamasia kutoka Wilaya ya Manyoni wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kwani yamewajengea uwezo wa kukagua na kutambua bidhaa ambazo hazina ubora.Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa pamoja na mambo mengine akizungumzia kuhusu baadhi ya majukumu ya TMDA kukasimishwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa TAMISEMI.

Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa akiwaelekeza jambo washiriki wa mafunzo hayo.

Mshiriki wa mafunzo hayo Upendo Kiula ambaye ni Mratibu wa Huduma za Maabara kutoka Wilaya ya Itigi, akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo.

Mshiriki wa mafunzo hayo Alfred Rwamtoga Mfamasia kutoka Wilaya ya Manyoni akizungumza kuhusu mafunzo hayo


Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Taswira ya mafunzo hayo.

Afisa wa TMDA, Neema Debwe akichukua moja ya matukio wakati wa mafunzo hayo. 

Mafunzo yakiendelea.Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo hayo na mgeni rasmi

No comments