MAAFISA WATENDAJI WATAKIWA AJENDA YAO KUWA ANWANI ZA MAKAZI, KUHAKIKI TAARIFA ZA WANANCHI
Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)
MAAFISA Watendaji wa Mitaa kote nchini wametakiwa katika vikao vyao vyote
vya msingi ajenda yao kubwa iwe ni anwani za makazi pamoja na uhakiki wa taarifa
za wananchi.
Ombi hilo limetolewa Machi 15, 2024 na Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH), Innocent Jacob wakati wa siku ya pili ya mafunzo ya siku 14 kwa watendaji wa kata, mitaa, wenyeviti wa Serikali za mitaa na vijiji yanayohusu namna ya kukusanya taarifa za Anwani za Makazi Manispaa ya Singida yaliyoanza Machi 14, 2024 ambayo yameandaliwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kuwa siku mbili kati ya hizo 14 zitatumika kwa ajili ya kuhakiki taarifa. .
Jacob alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawzesha wenyeviti hao ili waweze
kutoa taarifa kwa wanananchi za zoezi hilo ndani ya siku hizo na wananchi nao
waweze kutoa za kwao kama NIDA, namba ya simu, Tin namba ya biashara na taarifa
nyingine za majengo, makazi kama walivyoelekezwa watendaji wa mitaa jinsi ya
kulifanya zoezi hilo.
"Watendaji wa mitaa ndio watakao kwenda kukusanya taarifa hizi kwa
wakazi wao kwa sababu katika maeneo yote ya utawala wao ndio wahusika wakubwa
na watashirikiana na wenyeviti wa mitaa kufanya kazi hiyo," alisema Jacob.
Alisema Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH), kwa
kushirikiana na TAMISEMI, wameandaa zoezi hilo kwa lengo la kuhakiki taarifa za
makazi kwa awamu ya pili baada ya awali kufanyika kwa njia ya operesheni ambapo
huenda kuna baadhi ya wakazi hawakuweza kupata fursa ya kuingia katika
kanzidata ya Anwani za Makazi.
Alitaja baadhi ya vitu ambavyo viliweza kusahulika kuwekwa kwenye kanzidata
kuwa ni taarifa ya majengo, viwanja, majina katika vibao vya mitaa hivyo
kurudiwa tena katika zoezi hilo la awamu ya pili la uhakiki.
Jacob alisema umuhimu wa Anwani za Makazi zitarahisisha utambuzi kwa wakazi
wa eneo husika na kuweza kupata huduma mbalimbali kwa kufikiwa kiurahisi mahala
walipo kwa kutumia programu tumizi kwa ajili ya umma inayoitwa NAPA ambayo
inapakuliwa kupitia simu janja ambapo wananchi wote hapa nchini wakiwemo wa
Manispaa ya Singida wataweza kuingia katika mfumo huo kwa kuandika NAPA
Tanzania.
Alisema mafunzo hayo yanafanyika Manispaa ya Kigoma, Iringa na Singida na
yatakuwa endelevu kwa kufanyika katika mikoa mingine.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Dkt. Adrianus
Kalekezi alisema katika mafunzo hayo wataalamu wanaelekeza namna ya kuingiza
taarifa katika mfumo wa Anwani za Makazi na kuwa hivi sasa wanauhisha taarifa
za awali baada ya kazi hiyo kufanyika awamu ya kwanza.
Dkt. Kalekezi alisema suala hilo la Anwani za Makazi ni la muhimu katika
manispaa hiyo kwani wananchi watapata huduma kwa urahisi na alitumia nafasi
hiyo kuwaomba wananchi kuilinda miundombinu ya Anwani za Makazi iliyowekwa kama
vibao vinavyoonesha majina ya mitaa na barabara na kueleza kuwa ni lazima
ilindwe ili waweze kunufaika na zoezi hilo kwani bila miundombinu hiyo inakuwa
vigumu kwao kuelekezwa na kuitambua mitaa na barabara.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwankoko, Habiba Juma akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo alisema zoezi hilo litawarahisishia kutoa huduma kwa wananchi na kupunguza gharama ya fedha na muda kutoka sehemu moja kwenda nyingine na wananchi wataweza kupata huduma kupitia anuani za makazi.Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka WHMTH, George Leonard, akitoa mafunzo kwa watendaji hao.Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka WHMTH, Janeth Peter , akiwajibika wakati wa mafunzo hayo.Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Dkt. Adrianus Kalekezi, akizungumzia zoezi hilo.
No comments