SERIKALI KILOSA YACHUKUA TAHADHARI YA MAFURIKO
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka akizungumza wakati walipotembelea waathirika wa mafuriko yaliyotokea jana Machi 17, 2024 wilayani humo ambapo Kaya zaidi ya150 zimeathiriwa.
...........................
Na Dotto Mwaibale (Singidani Blog)
SERIKALI Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro imechukua tahadhari zaidi ili kuwafanya wananchi kuwa
salama baada ya kukabiliwa na mafuriko yaliyosababishwa na mto Miombo kujaa
maji kutoka milimani.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka akizungumza na waandishi wa
habari kwa njia ya simu Machi 18, 2024 alisema zaidi ya kaya 150 zimeathiriwa
na mafuriko hayo yaliyotokea jana Machi 17, 2024.
“Tunaendelea kuchukua tahadhari ili kuepusha madhara zaidi kwa wananchi
kwani bado maji yanateremka kutoka milimani kufuatia mvua kubwa iliyonyesha
jana,” alisema Shaka.
Shaka alisema kufuatia mafurika hayo mawasiliano ya barabara kati ya Mikumi
na Kilosa yamekatika na sasa wanajenga kivuko cha muda ili kisaidie kurahisisha
usafiri wakati ujenzi wa daraja jipya kubwa la kisasa likianza kujengwa na
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) baada ya Rais Samia Suluhu
Hassan kutoa Sh.Bilioni 1 kwa ajili ya kazi hiyo.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha za ujenzi wa daraja hilo ambalo
litakuwa likipitika wakati wote na kuinua uchumi wa wananchi wa Kilosa na Mikumi
na maeneo mengine,” alisema Shaka.
Shaka alisema tahadhari nyingine wanayoendelea kuichukua ni kudhibiti
magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kutokea kutokana mafuriko hayo.
Alisema awali Serikali ilipanga waathirika wote wa mafuriko hayo wapewe
hifadhi katika moja ya shule lakini familia zao ziliomba ziwape msaada huo.
Mara baada ya kutokea mafuriko hayo DC Shaka pamoja na Wajumbe wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama walifika maeneo ambayo yalikumbwa na mafuriko kujionea hali
halisi na kuchukua hatua za awali za kuwasaidia waathirika.
Aidha, DC Shaka na wajumbe wake hao walifika eneo la daraja linalounganisha vijiji vya Nyali na Nzumbo ambalo limechukuliwa na maji na kusababisha huduma za usafiri
kusimama.
Wakiwa kwenye eneo hilo walijikuta wamezingirwa na maji hivyo kulazimika
kuanza kuondoka kujinusuru huku wakitoa msaada kwa wananchi wengine ambao
walikuwa wamekwama kwenye makazi yao.
No comments