PROGRAMU YA IMARISHA UCHUMI NA MAMA SAMIA YAZINDULIWA MKOA WA PWANI
Mwenyekiti wa Jukwaa la Kiuchumi la Wanawake Mkoa wa Pwani, Mariam Ulega akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu ya ‘Imarisha Uchumi na Mama Samia’ mjini kibaha juzi.
.......................
Na Mwandishi Wetu, Pwani
BARAZA La Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limezindua programu kabambe ya ‘Imarisha Uchumi na Mama Samia’ lenye lengo la kuwawezesha wanawake, vijana na makundi maalum kujiunga na majukwaa ya kiuchumi ili kujishughulisha na ujasiriamali ili kujikwamua katika umasikini.
Akizungumza kwenye uzinduzi rasmi wa programu hiyo ya ‘Imarisha Uchumi na Mama Samia’ mjini kibaha juzi , Mshauri wa Rais wa Mambo ya Wanawake na Makundi maalum, Bi Sophia Mjema alisema kwamba progaramu hiyo maalum inafungua milango kwa wanawake, vijana na makundi maalum kujisajili na kuingia kwenye mfumo wa kieletroniki.
Alisema kwamba programu itawawezesha makundi hayo yote tajwa kuweza kupatikana kwa taarifa zao rasmi serikalini za kibiashara ili kwenda sambamba na utekelezaji wa sera ya kitaifa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Bi Mjema aliongeza kwamba mfumo huo wa kidigitali ambapo utaweka kanzidata na kupata takwimu ya idadi ya majukwaa ya kiuchumi ya wanawake ambapo watapata fursa ya kubadilishana uzoefu, kupanua wigo wa biashara na fursa mbalimbali.
"Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan akiwa makamu wa rais aliwezesha uanzishwaji wa Jukwaa la wanawake kiuchumi ili kuweza kumkwamua mwanamke kutoka kwenye umasikini na aweze kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali na kushiriki kwenye shughuli za uchumi na biashara kwenye nchini yao," alisema Bi Mjema.
Alisema kwamba ni nafasi ya wanawake kuchangamkia fursa zitakazotakana na programu hiyo kwa kuwahi kujiandikisha kwenye mfumo huo maalum ili kuweza kujulikana rasmi na serikali kuweza kupata nafasi ya kuwezeshwa kiuchumi na kupata fursa ya kupata ruzuku na mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha na mifuko ya ruzuku.
Bi Mjema aliongeza kwamba kwa sasa dunia ipo kwenye sayansi na tekonolojia ndio maana baraza hilo limeamua kuja na programu hii ya kieletroniki ili kuweza kupata takwimu sahihi ya wanawake na vijana nchini nzima lakini pia kutoa mwamko wa matumizi ya teknolojia kwa wajasiriamali hapa nchini.
Alifafanua kwamba ni muhimu pia kwa baraza kuendelea kuhamasisha wanawake kuendelea kujisajili na kuwatajarisha watanzania kushiriki kwenye biashara za ushindani na kuwajengea uwezo na mafunzo kuhusu shughuli mbalimbali za kiuchumi hapa nchini.
"Moja ya umuhimu wa programu hii ya ‘Imarisha Uchumi na Mama Samia’ ni pamoja na mambo mengine ni kuwatambua na kujua wanaendeleaje na shughuli zao za biashara kwenye maeneo yao,”
“Ukienda China kuna maeneo maalum yametegwa kwa ajili ya huduma na bidhaa fulani , nina imani ipo siku tutafika huko kwa sasa kibaha ni sehemu maalum ya viwanda tutumie fursa hiyo ya viwanda kuweza kufanya biashara na kutoa huduma kwenye viwanda," aliongeza.
Kwa Upande wake , Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi Beng’i Issa alisema kwamba programu hiyo ni maalum kwa ajili kuwatambua na kuwajengea uwezo wa kiuchumi wanawake , vijana na makundi maalum ili kuendana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwakwamua wanawake kiuchumi hapa nchini.
"Baraza hili lilianzishwa mwaka 2004 ikiwa na jukumu la kutunga sera , kutengeneza mikakati ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuhakikisha kwamba utekelezaji wa sera na miongozo hiyo inakwenda sambamba na kuwaondoa wananchi kwenye umasikini ," alisema Bi Issa.
Alisema kwamba jukumu moja la baraza hilo ni kuwawezesha wananchi kwa kuwapa taarifa, ujuzi kwa maana ya kutoa mafunzo mbalimbali na kuwaunganisha na taasisi za kifedha na mifuko ya ruzuku kwa ajili ya kupata fedha ili kuweza kufanya biashara zao kwa ufanisi zaidi.
"Baraza pia litaendelea kuwasaidia kuwaunganisha wanawake na vijana jinsi ya kupata mikopo na ruzuku kutoka kwenye taasisi za kifedha ingawa asilimia kubwa ya wanawake wajasiriamali hapa nchini hawapo katika mifumo rasmi ya kifedha kama kwenye benki ingawa kwa sasa kuna mifuko takribani 70 ya kutoa mikopo na ruzuku," alifafanua.
Bi Issa aliongeza kwamba programu hii ya Imarisha Uchumi na Mama Samia inatarajia kusajili wajasiriamali 62,000 kwa kuanzia na usimamizi utakuwa kwenye ngazi za wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya , manispaa na wadau husika lengo ni kuhakikisha majukwaa haya ya wanawake nchini nzima yanatambulika na kuingia kwenye kanzidata ya taifa ili kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi.
Alisema kwamba baraza lina jukumu ya kuratibu shughuli zote za uwezeshaji wananachi na kuwasaidia kuhusu mifumo ya kodi, sheria za nchini , kanuni na kuweza kuwasaidia katika changamoto za urasimu wa ufanyaji wa shughuli za kiuchumi hapa nchini.
Bi Issa alisema kwamba mfumo huo ni rahisi kwa wajasiriamali kujisajili kwa kutumia simu zao za kiganjani kama vile kama simu janja na aina zingine ambapo itairahisishia serikali kujua hali zao za kibiashara kwenye maeneo yao ya uzalishaji na kuweza kutoa miongozo mbalimbali ya serikali katika juhudi za kuwainua wanawake hapa nchini.
"kwa mkoa wa Pwani kuna majukwaa takribani 1901 ambayo yanafanya kazi ya kuwahamasisha wanawake kuingia kwenye shughuli za kiuchumi na kushiriki kwenye maonyesho mbalimbali ya kitaifa ambapo ni fursa kwao kuonyesha bidhaa na huduma zao katika juhudu za kupanua wigo wao wa biashara," aliongeza Bi Issa.
Kwa upande Dkt Elizabeth Mshote kutoka Ofisi Mkuu wa Mkoa Wa Dar es Salaam alisema kwamba ni muhimu kwa majukwaa hayo ya kiuchumi kuweza kutambua fursa zilizopo kwenye viwanda hasa Mkoa wa Pwani kwa kuzngumza na na wenye viwanda kuhusu kushirikiana nao kwenye miradi ya kijamii kama sehemu ya kurudisha faida yao kwa jamii.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wenyeviti na makatibu wa Majukwaa ya Wanawake kiuchumi kutoka Mkoa wa Pwani kutoka wilaya zote za mkoa huo , Kisarawe, Kibiti, Rufiji, Mkuranga, Bagamoyo, Chalinze na Kibaha Mjini.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi Beng’I issa (kushoto) akiteta jambo na Mshauri wa Rais Mambo ya Wanawake na Makundi Maalum, Bi Sophia Mjema wakati wa uzinduzi wa programu ya ‘Imarisha Uchumi na Mama Samia’ juzi kibaha.
Wanawake wa Majukwaa ya kiuchumi Mkoa wa Pwani wakishiriki mkutano wa siku moja wa programu hiyo.
No comments