BALOZI DKT. NCHIMBI ATAKA MAOFISA UTUMISHI KUACHA UONEVU
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Jchimbi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wataalam wa Rasilimali Watu na Utawala Duniani ambayo kitaifa yalifanyika Mkoa wa Morogoro Mei 20, 2024.
...................
Na Mwandishi Wetu, Morogoro.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi
amewataka watumishi wanaosimamia utawala na rasilimali watu sehemu za kazi
kuwatendea haki wafanyakazi wote kwa kujiepusha na vitendo vyovyote vya uonevu.
Akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wataalam wa Rasilimali Watu na
Utawala Duniani, leo Jumatatu, Mei 20, 2024, ambayo kitaifa imefanyika mkoani
Morogoro, Balozi Nchimbi amewataka watumishi wanaosimamia rasilimali watu na
utawala kujiepusha na uminyaji haki na kujali stahiki za wafanyakazi,
zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Aidha, Balozi Nchimbi amesema dhamana ya nafasi zao za kusimamia utawala na
rasilimali watu zitaendelea kuhitajika na kuheshimika iwapo baadhi ya watendaji
wanaoendekeza tabia ya kujifanya ‘miungu watu’, na kuweka mbele maslahi binafsi
katika ofisi wanazozisimamia, wataacha tabia hizo.
Katibu Mkuu huyo wa CCM ambaye ni mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo,
amewataka Wanachama wa Wanachama wa Chama cha Wataalamu wa Rasilimali Watu na
Utawala Tanzania (THRAPA), kila mmoja wao kujiona ana deni la kutoa utumishi wa
kusaidia wafanyakazi kupata haki na maslahi yao katika sehemu zao za kazi.
“Ni muhimu sana tukumbushane kuwa tuna dhima kubwa ya kusaidia kujenga na
kuimarisha nguvu kazi endelevu katika maeneo yetu ya kazi na kwenye ofisi zetu.
Taaluma yetu hii itaendelea kuhitajika na kuheshimiwa sana iwapo sote
tutatimiza wajibu wetu wa kuhakikisha watu wanapata haki na maslahi yao. Baadhi
yetu waache kujifanya miungu watu, wanaonea watu na kutisha watu. Unakalia
faili la mtu mwaka mzima. Tuache hizo tabia mbaya; alisema na kuongeza:
“Watu wapande madaraja yao kwa merits (sifa) zao, wapate vyeo kwa merits,
wapate safari kwa merits. Watu wapate madai yao, mishahara, posho, likizo…hizo
zote ni haki za watu. Tusimamie haki za watu bila haya. Msionee watu wala
kuleta undugu au kuomba rushwa ndiyo mtu apate haki na maslahi yake. Kila mmoja
wetu atambue analo deni la kutumikia watu kwa kutanguliza maslahi ya taasisi na
watu mbele, kuliko maslahi yake binafsi,” amesema Balozi Dk Nchimbi.
No comments