Breaking News

MCHUNGAJI KIBAHA AKOSHWA NA KASI YA MAENDELEO YA NCHI CHINI YA RAIS SAMIA

Mchungaji Emmanuel Lyimo wa Kanisa la Christian Mission Fellowship Tanzania.
 

................................

Na Mwandishi Wetu, Kibaha

MCHUNGAJI Emmanuel Lyimo wa Kanisa la Christian Mission Fellowship Tanzania lililopo Mtaa wa Pangani Kata ya Kidimu Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani amesema maendeleo makubwa yaliyofanyika kwa kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan sio ya kawaida hivyo ameomba watanzania kuendelea kumuombea aweze kuwa na afya njema na kufanya zaidi ya hapo kwa maslahi ya nchi.

Lyimo aliyasema hayo katika ibada ya kawaida ambayo ilifanyika Mei 5, 2024 sanjari na kuliombea taifa na viongozi wake ili Mungu aendelee kuimwagia baraka nchi ya Tanzania na kuendelea kuwa na amani na utulivu.

"Hata kama mtu hawezi kusikia basi atakuwa anayaona maendeleo makubwa yaliyofanyika katika sekta mbalimbali hapa nchini chini ya Rais Samia Suluhu Hassan," alisema Lyimo.

Alisema mafanikio haya yanafanyika ni  kutokana na baraka za Mungu ambazo ameipa nchi yetu ya Tanzania na si vinginevyo kwani tunaziona nchi nyingine zinavyopita katika wakati mgumu na kushindwa kupata  fursa kama tuliyonayo watanzania ya kuabudu kwa amani pasipo bugugha yoyote.

"Kuna wenzetu katika nchi nyingine wanatamani kwenda kuabudu lakini hawawezi kutokana na vita na mambo mengine lakini sisi wakati wote tunabudu kila mtu kwa imani yake na bila ya kutofautia," alisema Mchungaji Lyimo.

Alisema kama kiongozi wa dini hashindwi kuwaambia waumini wake kuhusu mafanikio yanayoonekana nchini kwani jambo hilo linampendeza hata Mwenyezi Mungu.

Mchungaji Lyimo aliwaomba watanzania bila ya kujali tofauti za dini na imani zao kuendelea kuiombea nchi yetu na viongozi wake ili amani na utulivu uliopo uendelee kutamalaki mbele ya Mwenyezi Mungu.


No comments