Breaking News

RC SINGIDA ATAKA KUUNDWA KWA MABARAZA YA WAFANYAKAZI

----------------------

Na Dotto Mwaibale, Singidani Blog

MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego amehimiza uundwaji wa mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi kwa ajili ya kusaidia kujua na kutatua changamoto zao.

Dendego ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema hayo wakati akihutubia katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (MEI MOSI) ambayo kimkoa yamefanyika Wilaya ya Ikungi na kuhudhuriwa na mamia ya wafanyakazi na wananchi wa wilaya hiyo.

Alisema mabaraza ya wafanyakazi ni ya muhimu na yapo kisheria na kama hayaitwishi kwa ajili ya kusikiliza kero za wafanyakazi hilo litakuwa ni kosa kama yalivyomakosa mengine.

Dendego alisema mabaraza ndio chombo cha kuwakutanisha wafanyakazi na wale wanaotakiwa kuyaanzisha wafanye hivyo   mara moja na kuwa yeye sio muumini wa watu wanaovunja sheria.

“Mabaraza haya yanafaida kubwa kama tutakaa nayo kwa sababu yanatupa ujumbe wa wale tunaowaongoza wanafikiri nini na sisi hapa tuliojuu tusione kwamba tunajua kila kitu hawa wadogo zetu tunaowaongoza nao  wanamawazo mazuri,” alisema Dendego.

Alisema vyama vya wafanyakazi havitakuwepo kwenye maeneo ya kazi kama bendera ni wajibu wa viongozi wa vyama hivyo kama walivyochaguliwa na wenzao kuhakikisha wanakuwa kiungo bora cha wale waliowachagua, waajiri pamoja na Serikali na kufanya kazi hiyo usiku na mchana kutetea maslahi halali ya wafanyakazi.

“Mimi kama mkuu wa mkoa na wadogo zangu wote ofisi zetu zitakuwa wazi masaa 24 kwa ajili ya kusikiliza madai halali ya wafanyakazi kwa kuwasiliana na kuzungumza na vyama ili kutatua changamoto zinazowakuta wafanyakazi.” alisema Dendego.

Dendego alisema mwishoni mwa mwaka huu utafanyika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mtaa hivyo aliwataka wana Singida hasa wanawake wenye sifa kujitokeza kwa wingi kuomba ridhaa ya kugombea nafasi za uongozi.

 Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Singida, Maria Bange alisema kila mwaka sherehe za maadhimisho hayo huambatana na kaulimbiu ambayo uchochea hali ya wafanyakazi kufanya kazi na kuwa  mwaka huu kaulimbiu hiyo inasema ‘ Nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafanikio bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha.

Bange alisema pamoja na kuwepo kwa kauli hizo kila mwaka bado baadhi ya waajiri wamekuwa na vikwazo vya kuvunja sheria kwa makusudi ikiwa pamoja na baadhi yao kutowaruhusu wafanyakazi wao kutojiunga na vyama vya wafanyakazi wa sekta husika kwa hofu kwamba watajua haki zao na kuzidai kwa waajiri.

Alitaja vikwazo vingine ni kwa waajiri kutowashirikisha  wafanyakazi wao katika majadiliano ya pamoja ambayo ni haki yao kisheria hivyo kushindwa kujadiliana namna ya kupata vitendea kazi, usafi na mazingira yote bora sehemu za kazi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Singida, Agnes Lucas alisema mshahara kwa mfanyakazi ndio chanzo cha msingi wa haki zake zote na kuwa mfanyakazi anapokwenda kufanyakazi nje ya ofisi yake atapangiwa posho yake kulingana na mshahara wake.

Lucas alisema kila jambo atakalolifanya mfanyakazi na atakapohitaji malipo yatafanyika kulingana na mshahara wake na hata atakapo maliza muda wake wa utumishi kitakachoangaliwa ni mshahara wake.

“Kwenye kile kitu kinachoitwa kikokotoo ambacho sasa hivi ni kiboko na mjeledi mkali kwa mfanyakazi kwani kila anayekisikia anasimama kwanza kutaka kujua kinasemweje na hapa leo wanasubiri kusikia wataambiweje kuhusu jambo hilo,” alisema Lucas.

Lucas alitumia maadhimisho hayo kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Singida,  Halima Dendego akawaombee kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiondoe kikokotoo hicho.

“Tunaomba kikokotoo kiondolewa kutokana na hali ya maisha ilivyongumu,” alisema Lucas huku akishangiliwa na wafanyakazi waliokuwepo kwenye maadhimisho hayo.

Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Lucy Boniface akitoa salamu za chama kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Martha Mlata alisema CCM kimeridhishwa na Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo alitoa shukurani kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anatoa fedha nyingi za kuitekeleza.

Kaimu Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kati ambayo inahudumia mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma, Mzee Kasuwi, akizungumza kwenye maadhimisho hayo kwa niaba ya Kamishna Jenelali wa DCEA nchini aliwahusia wafanyakazi na jamii yote kwa ujumla kuhusu changamoto ya dawa za kulevya nchini hasa katika eneo la kanda ya kati kuachana na uzalishaji, usambazi, biashara na matumizi ya dawa za kulevya kwani ni janga la kitaifa na dunia.

Alisema DCEA inafanya utekelezaji wa majukumu kwa kusimamia nguzo kuu nne ambazo ni kupunguza usambazi wa dawa za kulevya nchini, kupunguza mahitaji ya dawa za kulevya katika jamii.

Kasuwi alitaja nguzo nyingine kuwa ni kupunguza madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na kuimarisha ushirikiano na wadau kitaifa, kikanda na dunia katika udhibiti wa dawa za kulevya ikiwemo kutengeneza mikataba ya kimataifa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vinavyojishughulisha na udhibiti wa dawa za kulevya.

Kasuwi alitumia nafasi hiyo kuwaomba watanzania hususani wana Singida kushiriki kwa dhati katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa kuhusu wa zalishaji na wasambazaji wa dawa hizo pamoja na kuwatolea taarifa waraibu wa dawa hizo ili kuweza kupata usaidizi wa tiba na huduma za utangamao.

Katika maadhimisho hayo kulikuwepo na burudani mbalimbali kama michezo ya kuvuta kamba, sarakasi zilizofanywa na vijana wa Polisi Jamii wa Wilaya ya Ikungi na kutolewa zawadi kwa wafanyakazi bora, muajiri bora na kwa makundi mengine.Mkuu wa wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wafanyakazi yaliyofanyika kimkoa Wilaya ya Ikungi. Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Singida, Agness Lukas akizungumza kwenye maadhimisho hayo.Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Singida, Maria Bange akisoma risala ya wafanyakazi wakati wa maadhimisho hayo.Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga akizungumza kwenye maadhimisho hayo.Kaimu Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kati, Mzee Kasuwi, akizungumzia majukumu ya DCEA.Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Lucy Boniface akitoa salamu za chama hicho kwenye maadhimisho hayo.Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi,  Rashid Rashid akiwatambulisha viongozi wa wilaya hiyo waliohudhuria maadhimisho hayo.Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Lucy Boniface (kulia) akiteta jambo na Katibu wa TUCTA Mkoa Singida, Maria Bange. Kushoto ni Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Singida, Agness Lucas.Viongozi meza kuu wakishiriki kuimba wimbo wa mshikamano wa wafanyakazi.Wimbo wa mshikamano ukiimbwa.Wimbo wa mshikamano ukiimbwa.Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego akipunga mikono wakati alipokuwa akiyapokea maandamano ya wafanyakazi wakati wa maadhimisho hayo.Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO( wakipita na gari lao huku wakionesha shughuli wanazozifanya mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego.Maandamano yakipita mbele ya jukwaa kuu.Wafanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakipita mbele ya mgeni rasmi wakati wa maadhimisho hayo.Maandamano yakiendelea.Wafanyakazi wa Chuo cha Veta Dodoma wakipita mbele ya mgeni rasmi wakati wa maadhimisho hayo.Walimu kupitia CWT waklionesha furaha yao wakati wakipita mbele ya jukwaa kuu.Maandamano yakiendelea.Maonesho ya ususi yakioneshwa.Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye sherehe hiyo ya wafanyakazi.Taswira ya maadhimisho hayoWafanyakazi wa TANESCO wakiwa kwenye banda lao wakati wa maadhimisho hayo.Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Misuna wakitoa burudani.Kwaito likichezwa.Wafanyakazi wakionesha furaha yao huku wakiwa wameinua kofia zao.Twisti ikichezwa wakati wa maadhimisho hayo.Mchezo wa uvutaji kamba ukifanyika.Wanawake wakicheza mchezo wa kuta kamba.Kiongozi wa Polisi Jamii kutoka Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi, Dominick Shirima akionesha umahiri wa kuruka kichwa chini miguu juu wakati wa maadhimisho hayo.Polisi Jamii Joseph Mbua akionesha umahiri wa kucheza sarakasi.Polisi Jamii wakicheza mchezo wa kupita kwenye ringi lililowashwa moto.Pikipiki ikipita kwenye matumbo ya Polisi Jamii wakati wa maadhimisho hayo.Sarakasi zikioneshwa.na vifana wa Polisi Jamii wa Wilaya ya Ikungi.

Attachments area Preview YouTube video MEI MOSI, 2024 -YAFANA MKOANI SINGIDA

No comments