Breaking News

MAFUNZO YA KIROHO YANAHITAJI MIILI YENYE AFYA BORA

Na WAF – Dar Es Salaam

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya wa Wizara ya Afya Bi. Neema Joshua amesema masuala ya kiroho na kiimani yanabebwa na mwili kuwa na afya bora na utimamu wa akili.
Bi. Neema amesema hayo leo Julai 22, 2024 na wakati wa kikao kazi na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) jijini Dar Es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa vikao vya uhakiki na kupitisha maudhui ya jumbe yaliyopo kwenye rasimu ya mwongozo wa viongozi wa dini kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya masuala ya lishe nchini.
Amesema Wizara ya Afya inatambua ushirikiano uliopo baina ya viongozi wa dini kuhusu ya masuala ya Afya ikiwa ni moja ya juhudi zinazofanywa ambazo zimeleta mafanikio ya makubwa kwa kuwafikia watu wengi zaidi.
“Wizara ya Afya imeona Viongozi wa dini wana wafuasi wengi na wanaaminika kwa jamii pia wana mkono mrefu kuliko Serikali kwa sababu wanawafikia watu wengi, hivyo mkakati wa kuwatumia viongozi wa dini pamoja na kushirikiana nao kwenye kuhamashisha na kutoa elimu juu ya masuala ya lishe bora kwa jamii hivyo tunatamani uwe endelevu ili kuhakikisha tunakuwa na jamii yenye afya bora”. Amesema Bi. Neema.
Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa viongozi wa dini ndio wametumika toka kuanza kwa kuandaa muongozo huu hadi hivi sasa unapoelekea utekelezaji, na kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha kile kilicholengwa kiwafikie kweli wananchi.
Awali Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padri Dkt. Charles Kitima amesema dawa kubwa kuliko zote katika mwili wa binadamu ni lishe hivyo ameihakikishia wizara ya afya kuwa kwa kutumia jumuiya zao wanawafikia watu wengi na kueleza kuwa mtandao wa jumuiya za katoliki uko wazi hivyo wizara iwe huru kuwatumia ili kuifikia jamii.
“Zoezi linalofanyika la kutufikia viongozi wa dini lisiwe kwa sababu ni kwa ajili ya kupitisha huu muongozo , liwe endelevu, muwe mnafika katika Hospitali zetu na kupeleka wataalamu kwa ajili ya mafunzo ili tuweze kuhudumia watanzania walio wengi wanaokumbwa na magonjwa yasiyoambukiza ambayo husababishwa na kutozingatia mlo kamili". Ameeleza Padri Dkt. Kitima
Aidha, Padri Dkt. Kitima amemshukuru na kumpongeza Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwa kuwa kinara katika kupambana na uviko 19, na kuikaribisha Wizara kushirikana juu ya utoaji elimu ya masuala ya lishe bora kwa Watanzania.

No comments