Breaking News

RAIS SAMIA ATOA WITO WATANZANIA KULINDA MIUNDOMBINU YA BARABARA KWA MATUMIZI ENDELEVU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wasafirishaji wote nchini pamoja na Wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya barabara inayojengwa na Serikali kwa kutofanya shughuli za kijamii kama kulima, kuchimba pembezoni mwa barabara pamoja na kazi nyingine zinazoathiri barabara. 
Dkt. Samia ametoa wito huo Wilayani Kalambo mkoani Rukwa, leo Julai 16, 2024 mara baada ya kufungua barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port (km 107) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami. 

“Ujenzi wa barabara ni gharama sana, ukijenga kilometa moja ya barabara ni sawa na kujenga vituo vitatu vya afya pamoja na kuweka vifaa tiba ndani yake kwahiyo niwaombe sana tutunze barabara zetu”, amesema Dkt. Samia.

Dkt. Samia ameeleza kuwa kukamilika kwa barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port (km 107) kwa kiwango cha lami utasaidia kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa. 

Kabla ya barabara hii kujengwa nimeambiwa usafiri kuelekea Bandarini ilikuwa inachukua hadi siku nzima lakini baada ya barabara hii kujengwa ni masaa mawili tu umefika Bandarini Kasanga”, amesema Dkt. Samia.

 Dkt. Samia ameeleza umuhimu wa barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port na Bandari ya Kasanga kwani itasaidia kukuza utendaji wa biashara kwa kuwa inaunganisha nchi yetu na nchi jirani ya Zambia, DRC Congo na Burundi na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuzalisha kwa wingi ili miundombinu hiyo iweze kufanya kazi na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji. 

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameeleza kuwa barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port (km 107) ni sehemu ya mkakati wa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuunganisha miundombinu ya barabara pamoja na bandari zetu. 

Ameongeza kuwa tayari Rais Samia ameshatoa fedha kuanza ujenzi wa barabara ya Matai - Tatanda - Kasesya (km 50) ili kuja kuiunganisha na mtandao wa barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port ambayo ikikamilika itarahisisha usafiri na usafirishaji kutoka mpaka wa Kasesya na nchi jirani ya Zambia.

 Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa mkakati wa Serikali katika mwaka huu wa fedha 2024/25 ni kuanza usanifu wa barabara ya kutoka Laela - Mwimbi - Kizombwe (km 93). Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mohamed Besta ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port (km 107) kwa kiwango cha lami umekamilika mwezi Aprili, 2024 na umegharimu Shilingi Bilioni 150.5 ikijumulisha ujenzi, ushauri pamoja na fidia kwa wananchi. Besta ameeleza kuwa barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port (km 107) imetekelezwa na Mkandarasi China Railway 15 Group kwa kushirikiana na New Centry Company kutoka nchini China na umesimamiwa na Mhandisi Mshauri Kampuni ya Nicholas O’Dwayer.

No comments