Breaking News

WATANZANIA WAASWA KUTOA MAONI YAO DIRA 2050

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akizungumza na Wajumbe wa Tume ya Mipango na Timu Kuu ya Wataalamu  ya Dira ya Taifa 2050 ofisi kwake.

................................

Adelina Johnbosco, Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amewataka Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika zoezi la kutoa maoni yatakayowezesha kuandaliwa kwa Dira ya Taifa 2050.

Ametoa rai hiyo leo Agosti 28, 2024, ofisini kwake mjini Magharibi wakati akiongea na wajumbe wa Tume ya Mipango na Timu Kuu ya Wataalamu  ya Dira ya Taifa 2050 iliyoongozwa na mjumbe wa Tume ya Mipango na Mwenyekiti wa Timu hiyo, Dkt. Asha Rose Migiro.

“Watanzania wote waendelee kutoa maoni yao ili tuweze kupata Dira tunayoitaka, asitokee mtu tukishapata Dira akasema sikupata fursa ya kutoa maoni, makundi yote waone umuhimu wa kushiriki kutoa maoni, hili ni jambo muhimu na lenye manufaa katika kuisaidia nchi yetu,” alisisitiza Mhe. Abdulla

Vilevile, amehimiza ulazima wa kila Mtanzania kuhakikisha anadumisha amani na utulivu ili mipango ya maendeleo ya Dira 2050 iweze kutekelezwa kikamilifu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Abdulla, amewakaribisha Wananchi  wote  katika Chuo Kikuu cha Taifa cha  Zanzibar (SUZA), siku ya Jumamosi Agosti 31, 2024, ili kushiriki katika kongamano la kutoa maoni kwa ajili ya Dira ya Taifa 2050 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
Picha ya pamoja na wajumbe hao.
 

No comments