Breaking News

WAANDIKISHAJI WAPIGA KURA WATAKIWA KUZINGATIA MAELEKEZO YA TUME


Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Dkt. Zakia Abubakar akifungua mafunzo kwa watendaji hao ngazi ya mkoa kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa maafisa  yaliyoanza Septemba 14, 2024 katika Ukumbi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida.

HABARI PICHA / DOTTO MWAIBALE NA PHILEMON SOLOMON

( 0744 362990 )

MJUMBE wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Dkt. Zakia Abubakar amewataka Maafisa Uandikishaji Ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa Teknolojia ya Habari (TEHAMA) wa Halmashauri kuzingatia maelekezo yote yatakayo tolewa na Tume ili waweza kufanya kazi kwa wakati pindi zoezi la uandikishaji wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu litakapoanza.

Dkt. Abubakar ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa watendaji hao ngazi ya mkoa kuhusu uboreshaji wa Daftrai la Kudumu la Wapiga Kura kwa maafisa waliotajwa hapo juu mafunzo yaliyoanza Septemba 14, 2024 katika Ukumbi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida.

“Matokeo bora ya zoezi hili yatategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji Serikali, Vyama vya Siasa na Wadau wengine wa uchaguzi,” alisema Abubakar.

Abubakar aliwasihi maafisa hao kuwa na ushirikiano wa karibu na Tume wakati wote ambao watakuwa wakitekeleza majukumu yao  na watakapokuwa na jambo ambalo watahitaji ufafanuzi au changamoto yoyote wasisite kuwasiliana na Tume,” alisema Abubakar.

Mafunzo hayo yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata ambapo nao watatoa mafunzo hayo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao ndio watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni.

Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi endapo zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.

“ Nimejulishwa kuwa, baadhi yenu mlibahatika kushiriki katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Tume ikiwemo uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura katika awamu zilizopita kwa kutumia uzoefu mlionao na mafunzo mtakayopatiwa, ninaamini mtafanya kazi zenu kwa weledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hili,” alisema Dkt. Abubakar.

Dkt. Abubakar aliwasihi kutumia uzoefu walionao kuwasaidia wenzao ambao hawakuwahi kushiriki katika zoezi kama hili ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.Vilevile, wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.

Alisema jambo hilo ni muhimu kwani litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika, hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.

Mawakala hao hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni. Maelekezo zaidi kuhusu mawakala wa vyama vya siasa yatatolewa na wakufunzi na ni muhimu kuyazingatia.

Alisema kuwa Tume imetoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari kwa asasi za kiraia 157 na asasi za kiraia 33 kwa ajili ya uangalizi wa zoezi hilo hivyo ni muhimu kutoa ushirikiano kwa asasi hizo zitakapofika kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao na kuwa Tume itawapa vitambulisho kwa urahisi wa kuwatambua.

Dkt. Abubakar aliwasisitizia maafisa hao umuhimu wa kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa, vifaa hivvyo vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini.

Alisema kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivyo kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hilo muhimu na kuwa wanapaswa kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili waweze kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza.

Mshiriki wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Ester Chaula amesema katika Mkoa wa Singida wanategemea kuanza uboreshai wa Daftari la Wapiga Kura kuanzia Septemba 25, 2024 hadi Oktoba 1, 2024 ambalo litafanyika mkoa mzima.

Alisema katika Wilaya ya Singida zoezi hilo litafanyika katika vituo 167 kwenye jimbo moja la uchaguzi lenye kata 21 na kuwa maandalizi yote yamekamilika.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Naibu Uhamiji Mkoa wa Singida, Novati Dawson akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
Fomu zikijazwa
Washiriki wa mafunzo hayo wakijaza fomu

Mafunzo yakiendelea.
Viongozi wakiwa meza kuu
Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa Teknolojia ya Habari (TEHAMA) wa Halmashauri wakila kiapishwa.

No comments