Breaking News

WAZIRI MKUU: SUALA LA MAZINGIRA LIWE AJENDA YA KITAIFA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe ajenda ya Kitaifa na jukumu la kila mmoja kuanzia ngazi ya familia mpaka Taifa.

“Na tunapokwenda kuhifadhi mazingira lazima tuanze na ngazi ya familia na tunapopanda juu tupanue wigo hadi kwa wadau mbalimbali. Viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa na hii lazima iwe ajenda maalum, iwe ni ofisi za umma, za binafsi au kwenye taasisi.”

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 10, 2024) wakati akifunga mkutano maalum wa viongozi na wadau wa mazingira ulioitishwa ili kujadili mwenendo wa mazingira nchini. Mkutano huo ulifanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Amesema   kitendo hicho kitakuwa  ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuimarisha uhifadhi na Usimamizi wa mazingira nchini, kazi aliyoifanya kwa weledi, ustadi na mafanikio tangu akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Amemudu kusimamia na kutoa miongozo mahsusi ya kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa. Leo hii, yeye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunamuona anaendelea kulisimamia ili Taifa lifanikiwe katika uhifadhi wa mazingira kwa vizazi vya sasa na baadaye,” amesema.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo juu ya jitihada ambazo Rais Dkt. Samia amekuwa akizichukua ili kuhakikisha suala la nishati safi linakubalika.

"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuja na dhana mpya ya kukataa kukata miti na kutuhamasisha kuhusu nishati safi ya kupikia. Rais wetu amekuwa kinara wa nishati safi hadi na mwezi Mei alienda Ufaransa kuhutubia kuhusu nishati safi na yeye akiwa ni Mwenyekiti mwenza wa mkutano huo. Hii ni fahari kwa nchi yetu," amesema.

Amesema Serikali imetoa fursa kwa wajasiriamali kuanzisha biashara ya kuuza mitungi na majiko ya gesi hadi kwenye ngazi ya vijiji ili nishati hiyo iweze kupatikana kwa urahisi. “Huko mbele tutaweka ukomo wa matumizi ya mkaa na kuni,” ameongeza


 

No comments