MHE. PINDA AKUTANA NA VIONGOZI WA SERIKALI YA BOTSWANA JIJINI GABORONE
Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda (katikati) akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Kabo Morwaeng na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana Mhe. Dkt. Lemongang Kwape alipotembelea Ofisi ya Rais wa Botswana jijini Gaborone.
.......................................
Na Mwandishi Wetu, Boswana
Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, amekutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Mhe. Kabo Morwaeng na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
wa Botswana Mhe. Dkt. Lemongang Kwape alipotembelea Ofisi ya Rais wa Botswana
jijini Gaborone.
Mhe. Pinda amekutana na viongozi hao kwa lengo la kujitambulisha kama Mkuu
wa Misheni ya SADC na kuwatambulisha wajumbe wa misheni hiyo ambao wako nchini
Botswana kwa ajili ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliopangwa
kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024.
Mhe.Pinda aliambatana na Sekretarieti ya SADC, wajumbe wa SADC Organ
TROIKA, Baraza la Ushauri wa Uchaguzi la SADC, na Waangalizi wa SADC.
Mhe. Pinda aliwaambia wenyeji wake kwamba SEOM ipo Botswana tayari kwa
kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.
Mhe. Pinda aliisifu Botswana kwa maendeleo makubwa ya kiuchumi pamoja na
amani na usalama vilivyopo nchini humo, ambavyo vinaifanya Botswana kuwa bora
zaidi.
Pia aliwapongeza kwa kuwa wazalishaji wakubwa wa madini ya almasi na
kusaidia watu kutumia madini hayo halisi badala ya almasi bandia.
Kadhalika, aliwaambia wafikirie kuanzisha uzalishaji wa asali na bidhaa
zake, kwani wana misitu katika nchi yao ambayo wanaweza kuitumia kama biashara
kwa wakulima wao ili wapate kipato.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mhe. Kabo
Morwaeng, aliikaribisha SEOM nchini Botswana na kumhakikishia kwamba Serikali
ya Botswana iko tayari kufanya kazi nao na imejipanga vizuri kuhakikisha
uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu.
“Karibuni Botswana, hii ni nchi ya amani, na tumejipanga kuhakikisha
uchaguzi mkuu unakuwa huru na wa haki kwa kila anayeshiriki,” alisisitiza.
Alisema Serikali ya Botswana imejiandaa kwa uchaguzi mkuu na kwamba wako
tayari kwa uchaguzi na kuihakikishia SEOM kwamba uchaguzi utakuwa huru na wa
haki na kuendelea kudumisha amani na usalama katika nchi yao.
Akizungumza kwenye mkutano, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa wa Botswana, Dkt. Lemongang Kwape, aliahidi kwamba Botswana itafanya
Uchaguzi wake kwa amani na itaendelea kushirikiana na wanachama wengine wa SADC
kwa manufaa ya wote.
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.









.jpg)




No comments