WANA BUCHOSA MPIGIENI NGOMA YA BUGOBOGOBO MBUNGE WENU SHIGONGO KWA KUWALETEA MAENDELEO
Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo, akizungumza wakati wa kuhitimisha mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 jijini Mwanza.
---------------------------------------------------------
NYIMBO za jadi ni nyimbo zinazoimbwa na watu wa kabila fulani kama sehemu ya utamaduni wao, jamii huimba nyimbo hizo kama sehemu ya utamaduni wao lakini pia huwaburudisha kutokana na staili zao za uchezaji na huimbaji.
Nyimbo za asili zina umuhimu mkubwa katika maisha kwani humfanya mtu afurahie kwa kuwa katika kabila lenye nyimbo nzuri na za kuvutia.
Baadhi ya faida ya kuimba nyimbo za asili ni kuburudisha, kudumisha utamaduni, utambulisho wa jamii husika na taifa ambapo mtu huweza kumtambua kutokana na anavyoimba, kutumika katika kuwaenzi viongozi wao kutokana na kazi nzuri wanayoifanya na kutoa mafunzo kwa wengine.
Lengo la kuanza kuzungumzia umuhimu wa nyimbo za asili ni kutaka kuwaomba ndugu zangu Wana Buchosa kumpigia ngoma ya asili ya Kabila la Wasukuma ijulikanayo kama Bugobogobo Mbunge wao Eric James Shigongo kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kuwaletea maendele kuanzia sekta ya afya, elimu, kilimo, barabara, umeme na maji.
Ngoma hiyo ya Bugobogo ilikuwa ikitumika na inaendelea kutumika hadi leo kutoa burudani kwa viongozi wakiwemo machifu wa kabila la Wasukuma kama moja ya njia ya kuwapa heshima kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Mhe.Eric Shigongo wana Buchosa wanakupa hongera kwa kuwa mtumishi wao wa kweli na mtu atakayesema hajaona ulicho kifanya katika jimbo hilo atakuwa na sababu zake binafsi.
Wananchi wa Jimbo la Buchosa wanakila sababu ya kukupongeza kutokana na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa vitendo na uzalendo.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020 Shigongo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) alishinda kiti cha ubunge Jimbo la Buchosa kwa kupata kura 79,950 dhidi ya wagombea wenzake, Abbas Mayala (Chadema) – 11,285, Precedius Luhabuza (ACT – Wazalendo) – 637 na Felician Lutandula (CUF) – 317.
Nikiwa natembea kifua mbele nasema Shigongo ni tunu ya wana Buchosa na Taifa, hongera kwa kazi unayoifanya iliyotukuka ambayo kila mpenda maendeleo wa Jimbo la Buchosa na Tanzania kwa ujumla wanapaswa kuziunga mkono jitihada unazozifanya za kumsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwaletea maendeleo watanzania.
Mhe. Shigongo mara baada ya kuapishwa ndipo alipoanza kufanya mapinduzi makubwa ya maendeleo katika Jimbo la Buchosa na moja ya kazi aliyoifanya akiwa na siku 120 tu tangu aingie madarakani ni pale alipotembelea miradi ya maendeleo.
Miradi hiyo aliyoitembelea na kuzungumza na wananchi ipo Kata ya Bulyeheke.
Akiwa katika kata hiyo yenye jumla ya vijiji nane na vitongoji 34, alisema kwa kipindi kifupi tangu achaguliwe kuwa mbunge, kata hiyo ilikuwa imepokea jumla ya Sh.Milioni 227 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Fedha hizo pamoja na nguvu za wananchi zilitumika kwenye ujenzi wa zahanati, vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari, matundu ya vyoo, ofisi za walimu, wodi ya mama na mtoto ambapo miradi hiyo imekwisha kamilika.
Kazi nyingine aliyoifanya ni zaidi ya wananchi elfu 17 kati ya elfu 58 kwenye vijiji 8 Kisiwani Kome - Buchosa kunufaika na mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa na Kampuni ya Kamba's Group chini ya usimamizi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wenye thamani zaidi ya Bilioni 2.2.
Kufuatia kuharakisha maendeleo ya wana Buchosa kupitia mbunge huyo Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa kwenye ziara ya kikazi jimboni humo aliagiza uharakishaji wa ujenzi wa Barabara ya Sengerema Nyehunge yenye urefu wa kilomita 54.3 kwa kiwango cha lami kukamilika kwa wakati.
Dkt. Nchimbi alitoa agizo hilo Septemba 14, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Buchosa akitokea mkoani Geita.
“Ni muhimu sana kujiridhisha kuhusu uwezo wa wakandarasi kabla ya kupewa kazi na kufahamu historia zao za nyuma, kuna wengine tayari wanarekodi za kuharibu kila sehemu duniani waliko kwenda na kukimbilia kwetu kama sehemu ya kujifichia na kuja kutuharibia kazi," alisema Dkt. Nchimbi.
Shigongo kupenda kwake maendeleo ya vijana aliwataka kupambana kufa na kupona kuhakikisha wanatimiza ndoto zao na kufanikiwa maishani na kuwaeleza kuwa wakiwa maskini hakuna atakayewaheshimu.
Shigongo aliyasema hayo wakati wa kongamano la Knoswing Youth Purpose lililofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma, lililokuwa na lengo la kuwaongezea vijana uwezo wa kutambua vipawa vilivyomo ndani yao na kuwapa hamasa ya kutimiza ndoto zao.
Aidha, aliwataka vijana hao kutambua kwamba safari ya mafanikio ni ngumu na lazima wajitume kwa nguvu na uwezo wao wote ili baadaye waje kuishi maisha ya ndoto zao.
Shigongo katika kujiongezea elimu ili aweze kuwatumikia vema wananchi alitajwa kuwa miongoni mwa wanafunzi bora watatu waliohitimu Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO) kwenye kozi ya Shahada ya Kwanza ya Mawasiliano ya Umma (Bachelor of Arts in Mass Communication) mwaka 2020.
Kuonesha ni kiongozi anashughulika na kazi za kijamii alizindua mradi wa kituo kitakachosaidia kuondoa changamoto zinazoikabili jamii nchini hususan maeneo ya vijijini, uliotambulishwa kwa wananchi wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Mradi huo ambao upo chini ya Taasisi ya “Kijiji” unatekelezwa katika Kijiji cha Kasisa Jimbo la Buchosa, wilayani Sengerema na umebuniwa na Familia ya Aliyekuwa Mbunge wa Kwanza wa Kuchaguliwa Jimbo la Sengerema kati ya mwaka 1965-1985, marehemu Alphonce Rulegura, ili kuenzi nia yake njema ya kuwawezesha wananchi wa jimbo hilo kuondokana na umaskini.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Taasisi hiyo, Shigongo alisema mradi huo utaleta faida kubwa sio tu kwa wanakijiji wa Kasisa na maeneo jirani lakini pia nje ya Jimbo la Buchosa.
Shigongo anayeyaelewa mahitaji ya wana Buchosa kama mwakilishi wao Bungeni, amekuwa akiuliza maswali yenye tija ili kupeleka mbele maendeleo katika sekta mbalimbali.
Moja ya maswali hayo ni lile alilo uliza ni lini serikali itakamilisha uchimbaji wa visima vya maji vilivyoanza kuchimbwa Jimbo la Buchosa na kujibiwa na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi aliyesema serikali inaendelea na zoezi la utafiti wa maji ardhini pamoja na uchimbaji wa visima 13 kwenye jimbo hilo.
Majibu ya Naibu Waziri wa Maji, Mahundi yalitolewa Februari 13, 2024, Bungeni jijini Dodoma.
Aidha, Mbunge Shigongo ameelezewa kuwa ni kiongozi mwenye huruma kwa jamii hasa kwa watu wenye uhitaji maalumu wakiwemo watoto na kuwa utashi huo wa kusaidia jamii upo kwenye damu.
Mbunge huyo amekuwa akisaidia jamii tangu alipokuwa akichapisha Magazeti Pendwa ya Uwazi, Ijumaa, Amani, Ijumaa Weekenda, Risasi na mengineyo akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers Ltd.
Kutokana na kuwiwa kwake kusaidia makundi hayo yenye huhitaji ofisi yake ya Buchosa kupitia kamati ya kuhamasisha wazazi kupeleka watoto shule, aligawa sare za shule na madaftari kwa wanafunzi wanaotoka kwenye familia duni zisizo na uwezo pamoja na watoto yatima.
Zoezi hilo lilifanyika katika Shule ya Msingi Katwe, jimboni humo kwa kamati hiyo kushirikiana na Diwani wa Kata ya Katwe, Maximillian Mkungu, pamoja na uongozi wa shule na serikali za vijiji.
Mbunge Shigongo kufuatia kuwa na bidii ya kuwaletea maendeleo wanananchi wa jimbo lake Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alitoa fedha zaidi ya Sh.Bilioni tatu ndani ya kipindi cha miezi mitatu kwa ajili ya maendeleo.
Shigongo alitumia mkutano wa vijana wa CCM uliohudhuriwa na Rais katika Uwanja wa Nyamagana kumshukuru kwa fedha hizo alizozitoa kwa ajili ya wananchi wa jimbo lake.
Mbunge huyo amefanikiwa kuyafanya hayo yote kutokana na ushirikiano baina yake na viongozi wa Mkoa wa Mwanza, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Jumuiya zake, wataalamu pamoja na wananchi.
Imeelezwa kuwa, upole, ucheshi, kujishusha kwake kwa wananchi na kusikiliza kero zao na mahitaji yao kupitia mikutano ya hadhara anayoifanya ni jambo lingine linalomfanya afanikiwe huku wengi wakimtaja kuwa ni kiongozi anayewajali na mwenye huruma.
Aidha, mafanikio hayo makubwa yaliyofanyika katika jimbo hilo yametokana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.
Mbunge Eric James Shigongo nasema endelea kuwapelekea maendeleo wana Buchosa ambao kwa kazi hiyo kubwa uliowafanyia hawana deni na wewe zaidi ya kukushukuru kwa kukupigia Ngoma ya Bugobogobo.
Kwa leo niishie hapa nikutakie afya na kazi njema ya kuwatumikia wana Buchosa na Taifa kwa ujumla. Kazi Iendelee...
Imeandaliwa na Dotto Mwaibale, (0754-36 2990)




No comments