Breaking News

RC DENDEGO AZINDUA PROGRAMU ZA SHAHADA YA UZAMILI KATIKA MAHAFALI YA 22 TIA SINGIDA

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Programu ya Shahada za Uzamili ilioanzishwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wakati wa Mahafali ya 22 ya taasisi hiyo Kampasi ya Singida yaliyofanyika Novemba 22, 2024. Kutoka kushoto wanaoshuhudia tukio hilo ni Mjumbe wa Bodi ya Ushauri Wizara ya Fedha, Renatus Msangira, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TIA, Prof. William Pallangyo. 

Na Mwandishi Wetu, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ameongoza uzinduzi wa Programu za Shahada ya Uzamili iliyoanzishwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dendego aliipongeza taasisi hiyo kwa kuanzisha programu hiyo ambayo ni ya muhimu na akawaomba wana Singida na Wananchi wengine kuichangamkia na kueleza kuwa hiyo ni fursa kubwa kwao..

Ninayo furaha kubwa kuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya Ishirini na Mbili ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania, mahafali ambayo yanafanyika katika kampasi yetu ya Singida kwa mara ya Kumi na Tatu.

" Ninatoa shukurani zangu za dhati kwa Bodi ya Ushauri ya Wizara na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania, kwa kunialika kushiriki na kuwa Mgeni Rasmi. Tangu nilipowasili, nimepokelewa kwa heshima na ukarimu mkubwa, " alisema Dendego.

Dendego alipongeza kazi kubwa inayofanywa na taasisi hiyo, Bodi ya Ushauri, na Uongozi wake wakiwemo watumishi kwa kusimamia vyema utekelezaji wa malengo ya Taasisi kupitia Mpango Mkakati wake hususan katika utoaji wa mafunzo, tafiti, na ushauri wa kitaalamu kwenye nyanja mbalimbali.

Aidha aliipongeza TIA kwa kufanyia kazi maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kwa kutoa elimu ujuzi inayowawezesha wanachuo kujiajiri na kuzingatia kwa umakini suala la umahiri katika mitaala kwa lengo la kupata wataalam wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi.

 

Dendego alisema amevutiwa na juhudi za Mhadhiri Msaidizi wa taasisi hiyo Mary Kayanda katika kuboresha somo la Hisabati shule za Singida na kueleza kuwa huo ni mfano bora wa ubunifu na mchango wa Chuo hicho katika elimu na akatoa mapendekezo mkakati huo uendelee na ujumuishwe na masomo mengine ya Biashara kama Bookkeeping na Commerce, ili kuimarisha ujuzi wa wanafunzi.

"Nimesikia katika taarifa ya Mtendaji Mkuu Profesa Pallangyo kwamba watawatunuku wahitimu 1,477 hii ni faraja kubwa kwa Mkoa wetu wa Singida na Taasisi yetu ya Elimu hivyo nitoe wito kwa wahitimu kuwa, ingawa kuajiriwa ni fursa nzuri, kujiajiri ni bora zaidi, kwani inawapa nafasi ya kuwa wabunifu na uhuru wa kufikia malengo yenu, " alisema Dendego.  

No comments