Breaking News

SHIRIKA LA ENGENDERHEALTH LAIPA KONGOLE SERIKALI


 Mratibu wa Shirika hilo Mkoani Tanga Loveness Malisa akizungumza

........................................

Na Mashaka Kibaya

SHIRIKA la EngenderHealth Tanzania limeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii ikiwemo ya watu wenye Ulemavu kutokana na hatua yake ya kujenga vituo vingi vya afya hapa nchini .

Mratibu wa Shirika hilo Mkoani Tanga Loveness Malisa ametoa Shukrani hizo Jana katika risala yake aliyoitoa kwenye maadhimisho ya siku ya watu wenye Ulemavu yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa YPCP katika Jiji la Tanga.

Licha ya hayo Malisa alisema kwamba wanakutana na changamoto ya uwepo wa idadi ndogo ya watumishi waliopata mafunzo kuhusu huduma jumuishi na shirikishi kuhusu Kada ya watu wenye Ulemavu hivyo kuwasababisha kushindwa kufikia malengo.

Changamoto nyingine ni juu ya uwepo wa mifumo ya ukusanyaji wa taarifa za afya ambazo zimeshindwa kuwatambua watu wenye ulemavu hali inayokwamisha kuwafahamu watu wenye ulemavu wanaopata huduma .

Ameishauri Serikali kuweka mafunzo ya huduma shirikishi kwenye mitaala ya mafunzo kwa wanafunzi wa Kada ya afya sanjari na suala la uboreshwaji wa miumdombinu kwenye vituo vya afya kuifanya kuwa rafiki kwa walemavu.

Mmoja wa washiriki wa Mkutano huo Salehe Mwaluku ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuendelea kutoa elimu ya ujasiriamali kwa jamii ya watu wenye Ulemavu hatua ambayo itawawezesha kunufaika na fursa ambazo zinapatikana nchini kwao.

Amewasilisha ombi hilo wakati akichangia mada kwenye  Kongamano hilo lililoshirikisha wajumbe kutoka vyama vya watu wenye Ulemavu akisema, kuna haja kwa Serikali kuendelea kutoa elimu ya ujasiriamali  itakayowasaidia kumudu suala la utejeshaji Mikopo ya asilimia kumi.

Maadhimisho ya siku ya watu wenye Ulemavu Duniani hufanyika kila Disemba 3 kila mwaka lengo likiwa kukuza uelewa juu ya haki na ustawi wao na kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa kuwashirikisha walemavu kwenye nyanja zote za maendeleo kama vile afya.

Malengo mengine ni pamoja na kutathimini maendeleo katika utekelezaji sera na mikakati ya kuhakikisha usawa na ujumuishi kwa walemavu, pia ni jukwaa maalum lankuwaonesha watu wenye Ulemavu kuonesha vipaji vyao na kueleza changamoto wanazokutana nazi katika maisha yao ya kila siku.

No comments