Breaking News

MBETO : UKWELI UKUDHIHIRIKA UONGO HUJITENGA

 

Katibu  wa Kamati  Maalum  ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis,  akizungumza na Waandishi  wa habari  katika Òfisi Ndogo ya CCM  huko  Chachani Kisiwani  Pemba.

............................................ 

Na Mwandishi  Wetu, Pemba 

CHAMA Cha Mapinduzi  (CCM) kimesema  zama za ushindani wa siasa  usiotoa matokeo chanya, tija wala manufaa kwa  jamii zimepitwa na wakati  ,badala yake  wananchi wanataka kuona mambo kwa macho na vitendo .

Maneno  hayo yamebainishwa na Katibu  wa Kamati  Maalum  ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo  ,Khamis Mbeto Khamis,  alipozungumza na Waandishi  wa habari  katika Òfisi Ndogo ya CCM  huko  Chachani Kisiwani  Pemba.

Mbeto  yupo  Kisiwani  Pemba kuhudhuria Sherehe  za Maadhimisho  ya Miaka 61 ya Mapinduzi  Matukufu ya Zanzibar .

Alisema kadri siku zinavyozidi kwenda  mbele  ,toka  kizazi kimoja hadi kingine , wananchi wa  Zanzibar  ,wamekuwa wakibadilika polepole  huku wakiachana na siasa za kukaririshwa mambo  yasio fikirika.

"Zile zama za watu  kukaririshwa au kulishwa maneno yenye  siasa za  sumu    , chuki na hasama ,zinaelekea  kufikia tamati . Kila mtu   zanzibar sasa ameamka ,anataka kushuhudia kwa vitendo na kuona kwa macho yake " alisema Mbeto.

Katibu  huyo mwenzi ,alisema utawala wa Rais  Dk Hussein Ali  Mwinyi  tokea ashike madaraka, amekuwa kiongozi wa vitendo,  asiyeamini katika hadithi za kufikirika  zisizoipatia  jamii  manufaa na matunda ya maendeleo .

'Hatutaki siasa domo mtindi samli kwa mwenye ng'ombe. Wananchi  ni werevu wangependa  kuona  vitendo na kwa  macho yao.  Simulizi za nikipata nitafanya hazina nafasi . Watu wanataka kuona  aliye madarakani anafanya nini na kuonekana" alieleza Mbeto

Aidha    Katibu  huyo  mwenezi amewashauri Waandishi wa  vyombo mbalimbali vya habari  waliofika pemba kabla au baada ya sherehe  za Mapinduzi  ,waitembelee pemba na kushuhudia ustawi mpya wa  maendeleo  .

'Mwaka 2025 ni Mwaka wa kufunguliwa  milango ya kiuchumi na ongezeko la kasi ya maendeleo  pemba. Utajengwa uwanja   wa kisasa wa Ndege Chakechake . Bandari za Mkoani, Wesha na Wete " alisisitiza.

Mbeto alisema kuna ujio wa  Wawekezaji wa ndani  na nje  ambao watajenga Viwanda Vidogo ;Vya kati na Vikubwa Unguja na Pemba .SMZ imepania kuimarisha   sekta ya Uvuvi kwa kununua meli  zitakazofika masafa ya mbali  baharini.

Pia  aliwatolea wito  wanamichezo kisiwani Pe mba ,wakiwemo wanasoka, wanariadha,  wachezaji wa mpira wa pete, masumbwi ,  kuogelea ,wasanii wa muziki wa kizazi kipya na taarabu ,kuonyeaha  vipaji  vyao na kufikia  ngazi za  kimataifa.

'Siku zote ukweli ukidhihiri uongo utajitenga. Vitendo hunena  kuliko maneno  . Waacheni wapinzani  wetu  wabeze  maendeleo yaliopo huku  wananchi wakijionea  yote yanayofanyika" Alieleza  Mwenezi  huyo.


No comments