Breaking News

MASHEIKH, WANAZUONI WANOGESHA MAULID YA JUMUIYATUL ISLAMIYA PANGANI TANGA


.........................................

Na Mashaka Kibaya, aliyekuwa Pangani.

ILE siku ya jambo kubwa la kiimani imehitimishwa kunako Usiku wa Februari 14, 2025, kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu kukusanyika Wilayani Pangani, kwa ajili ya kusherehekea Maulidi ya kumbukizi ya kipenzi chao, Mtume Muhammad (SAW).

Sherehe hizo ziliongozwa na taasisi ya Jumuiyatul Islamiya chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ustaadh Rajabu Abdarahman Abdallah, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tanga na mjumbe wa kamati kuu wa Chama hicho kinachoshika dola.

Katika Sherehe hizo, mamia ya Waumini wa Dini ya Kiislamu waliweza kuhimizana mema na kukatazana mambo yaliyo mabaya huku upendo na amani vikichukua nafasi kubwa katika kuhubiriwa.

Mbali na hayo, suala la kuombeana heri kwa Mwenyezi Mungu, halikutupwa mkono, kwa vile waumini waliokusanyika walikumbushana kumwombea Dua Rais Dkt Samia Suluhu Hassan akitajwa kuwa Kiongozi aliyefanya mambo mengi makubwa katika kuharakisha maendeleo ya Watanzania walio wengi.

Imekuwa ni Jambo la kawaida na muhimu kwa Jumuiyatul Islamiya kuadhimisha Maulid haya, ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka na kwa mwaka huu wageni mbalimbali hususani Masheikh kutoka ndani na nje ya Mkoa walikuwepo.

Sheikh wa Mkoa wa Tanga Ally Juma Luwuchu kama Kiongozi na Sheikh wa wilaya ya Pangani walijumuika na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam 'Waridi' wengine kutoka taasisi mbalimbali za dini hiyo zilizopi Jijini Tanga na pia wale wa nje ya Mkoa huo hivyo kufanya Sherehe hizo kupambwa na sura zilizokuwa za kipekee.

Katika Sherehe hizo Mgeni rasmi alikuwa Issa Haji Gavu ambaye ni Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye alilieleza kusanyiko hilo ni muhimu na adhimu huku alidokeza umuhimu wa sherehe za Maulid kwa Waislamu.

Gavu alimwelezea, Mtume Muhammad (SAW) kuwa ni Kiongozi wa haki na nuru ya ulimwengu, huku akimtaja Muhammad (SAW) kuwa ni Kiongozi muadilifu katika umma uliosalia. Gavu aliwasihi Waumini kupendana.

Gavu alisema, katika Taifa la Tanzania, kuna watu ambao ni waumini wenye imani tofauti za dini huku akisisitiza kuvumiliana na juwataka waislamu kuishi kwa msingi wa amani na upendo wakati wote.

Kuhusu uchaguzi Mkuu wa Rais,wabunge na madiwani, Gavu alisema, ni vyema watu kuendelea kumuomba Mungu ufanyike kwa usalama pasipo kuwepo mifarakano kama ambavyo imekuwa ikitokea kwa baadhi ya mataifa.

Viongozi wengine wa Kiserikali waliohudhuria kmhadhara hiyo ni Waziri wa Maji na mbunge wa Pangani Jumaa Hamidu Aweso, ambaye alishiriki vyema kwenye mambo ya kiimani siku hiyo akiongoza kumswalia Mtume Muhammad (SAW) na kuwasihi waislamu kumuombea dua Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Aweso alisema, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni Kiongozi aliyeifanyia mema Tanzania na huku akiweza kuitoa pangoni wilaya ya Pangani ambayo awali iligubikwa na changamoto nyingi kwenye maendeleo.

"Uchapakazi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan umeibadili Pangani kwenye sekta za elimu,afya,Maji na hata miumdombinu ya barabara, Rais Samia ameitoa Pangani pangoni" alisema Jumaa Aweso.

Ametumia wasaa huo kuwataka waumini wa dini ya Kiislamu kumuombea Rais huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuendelea kuwa na afya njema na kumudu kuwatumikia Watanzania.

Aidha Ustaadh Rajabu Abdarahman Abdallah ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Jumuiyatul Islamiya, alisema kuwa, hakuna haja kwa watu kushangaa pale Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anapozungumzwa kwenye mikusanyiko ikiwemo ile yenye mitazamo ya kiimani.

Alisema, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa Kiongozi mahiri na kinara katika kuimarisha amani na utulivu mazingira ambayo yamekuwa wezeshi kwa wananchi kuendelea na shughuli nyingine za kuharakisha maendeleo.

"Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ametufanyia mambo mengi hususani watu wa Tanga, hakuna ubaya kuzungumzwa.Pia niwaeleze Rais atapita wilaya zote za Mkoa wa Tanga Februari 22 hadi mwisho wa mwezi" alisema Rajabu Abdarahman Abdallah Katibu Mkuu Kiongozi wa Jumuiyatul Islamiya na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga.

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoani Tanga alitumia fursa hiyo kuwataka Wananchi waliopoteza kadi zao za kupiga kura kwenda kujiandikisha kwenye daftari husika huku akisema iko haja kwa kila mmoja kumhamasisha mwenzake kujiandikisha.

Haji Sunday Manara ni miongoni mwa watu maarufu waliohudhuria hadhara hiyo akiwa ameambatana na Baba yake mzazi Mzee Manara.Haji alikabidhiwa jukumu la kuwa msema chochote 'MC' ambaye alionesha umahiri mkubwa katika kusoma Aya za Qur'an na kuongoza vyema shughuli ya kiimani.

Shughuli hiyo Maulid ya kumsifu Mtume Muhammad (SAW) iliyoratibiwa na Jumuiyatul Islamiya ilianza Februari 12, na kuhitimishwa Febr 14.

 Katibu Mkuu Kiongozi wa Jumuiyatul Islamiya Ustaadh Rajabu Abdarahman Abdallah ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga. akizungumza
Matukio mbalimbali katika maulid hayo
Taswira ya maulid hayo.
Vijana wakionesha umahiri wa kucheza kaswida
Viongozi wakiwa kwenye maulid hiyo
Maulid hiyo ikiendelea
Maulidi hiyo ikiendelea.


No comments