Breaking News

PROFESA KABUDI AVIPONGEZA VITUO VYA REDIO

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi (katikati) akiwa na viongozi wengine wakati akifungua mkutano mkuu wa watoa huduma za Utangazaji 2025 uliofanyika Februari 13, 2025, Kutoka kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui TCRA, Saida Muki, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rosemary Senyamule, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabir Bakari na Katibu Mkuu Wizara ya  Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji wa Serikali, Geryson Msigwa.

................................... 

Na Dotto Mwaibale, Dodoma

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amevipongeza vituo vyote vya redio kwa kazi nzuri ya kuhabarisha umma wakati wote wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi (Misheni 300) uliofanyika tarehe 27 – 28 Januari, 2025 jijini Dar es Salaam.

Profesa Kabudi alitoa pongezi hizo  wakati akifungua mkutano mkuu wa watoa huduma za Utangazaji 2025 ulioanza Februari 13 na kufikia tamati Februari 14, 2025 jijini Dodoma ambao unafanyika katika maadhimisho ya siku ya Redio Duniani.

Alisema  kupitia redio dunia ilifahamu kuhusu mkutano huo muhimu ulioongozwa na mwana mazingira namba moja Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“ Kipekee nitumie fursa hii kuvipongeza vituo vyote vya redio kwa kazi nzuri ya kuhabarisha umma wakati wote wa Mkutano huo ambao likuwa ni wa muhimu,” alisema Kabudi.

Aidha, Kabudi amevipongeza vituo vya redio vinavyorusha vipindi maalum vya kuhamasisha utunzaji wa mazingira hasa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa kuwa kinara wa kuandaa vipindi vya kutoaelimu ya utunzaji wa mazingira kama vile: Jambo Tanzania (27 ya Kijani), Kampemi ya Pika Kijanja inayosimamiwa na BONGO FM na kipindi maalum cha kuhamasisha usafi wa Mazingira (Jicho la Mpita Njia) ambavyo vimekuwa chachu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira hapa nchini. 

“ Kama mnavyofahamu, mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na tabia nchi ni ajenda muhimu kitaifa na kimataifa ambayo inaathiri maisha ya mwanadamu siku hadi siku. Mabadiliko ya tabia nchi yameweza kuathirimakazi ya watu pamoja na sekta ya kilimo na ufugaji kwa kiwango kikubwa,” alisema Kabudi.

Alisema uzalishaji wa mazao kwa ajili ya chakula umeathiriwa kutokana na mabadiliko ya misimu ya mvua sambamba na ongezeko la joto duniani.

Alisema ili wananchi waweze kuchukua tahadhari mapema Redio imekuwa ni chombo muhimu chenye kutoa taarifa kwa Wananchi.

Aliongeza kuwa utangazaji kupitia redio umekuwa na nguvu duniani kwa vile matangazo yake hufikia watu wengi, kwa haraka na gharama nafuu kuliko chombo chochote cha Utangazaji.

Alisema moja ya sababu ni unafuu wa kununua redio za kusikiliza ambapo wananchi wa hali ya chini, hali ya kati na hali ya juu kiuchumi wanaweza kumudu kununua chombo hiccho.

“ Kwa sasa redio nzuri zenye viwango vizuri hupatikana hata kwa bei ya Shillingi elfu kumi na tano (15,000/=). Hivyo basi, kwa vile redio ni chombo kinachomilikiwa na watu wengi duniani, na mimi pia niungane na kauli mbiu iliyotolewa na umoja wa mataifa ya kuhakikisha kuwa tunakuwa na vipindi vya redio vinavyotoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema.

Alisema Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa ni miongoni mwa nchi chache Afrika yenye vyombo vya kisasa vya kutabiri mwenendo wa hali ya hewa nchini na duniani. Kupitia jukwaa hili, nitoe wito kwa vituo vyetu vya utangazaji kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi pamoja na wakulima kuhusu utabiri wa hali ya hewa.

Profesa Kabudi akikumbusha umuhimu wa taaluma ya Utangazaji nchini na duniani kote alisema utangazaji umekuwa ukitumika kuleta umoja miongoni mwa jamii na taifa.

Alisema pamoja na jukumu la kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha, Serikali nyingi duniani zimekuwa zikitumia vyombo vya habari na utangazaji kuwasiliana na Wananchi wake kuhusu programu mbalimbali za kitaifa na kuhamasisha ushiriki wa Wananchi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema redio ni chombo muhimu sana katika kufikisha habari sahihi kwa wananchi ili kulinda maadili na usalama wa Taifa lolote duniani.

Alisema utangazaji usiozingatia weledi ulivyosababisha mifarakano, machafuko na mauaji kwenye maeneo mbalimbali duniani.

Alisema  Serikali zilizopo madarakani zimekuwa zikitumia vyombo hivi kama nyenzo ya utulivu na kupata mrejesho na maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu ujenzi wa taifa lao. Kwa kifupi utangazaji ni kiungo muhimu kati ya Serikali na Wananchi katika kuhamasisha amani, mshikamano na ujenzi wa Taifa.

Akijikita zaidi katika eneo hilo la utangazaji alisema huanzia kwenye maandalizi ya vipindi kwa kutambua lengo la kipindi na kuhakikisha kuwa maudhui utakayopeleka kwa hadhira itakayokusikiliza yanavutia na yameandaliwa kwa weledi mkubwa.

Alisema utangazaji huendana na sauti inayovutia, yenye kutamka matamshi kwa ufasaha lakini vilevile uwepo wa matumizi fasaha ya lugha unayotumia kutangaza.

“ Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kutumia taaluma yetu kwakuandaa vipindi vyenye tija kwa jamii na kuchochea maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya lugha yetu adhimu ya Kiswahili,” alisema Kabudi.

Akizungumzia katika eneo la maudhui ya vipindi vinavyorushwa na vituo vyetu, alisema bado hatujafanya vizuri sana na kueleza kuwa  vipindi vigi vina maudhui na ujumbe unaofanana na pia vimejielekeza katika utangazaji wa matukio na michezo hususan muziki, badala ya kuelimisha.

“ Redio nyingi hapa nchini bado hazijawa na vipindi vya kutosha vinavyotoa elimu mbalimbali kwa jamii na badala yake zimejikita kwenye burudani za muziki na mchezo wa mpira wa mguu. Pamoja na kuwa burudani ya muziki na michezo ni kitu muhimu kwa jamii, bado hakujawa na uwiano mzuri kati ya vipindi vya kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha< “ alisema Kabudi.

Alisema kimsingi, uwiano huo uko kwenye Kanuni za Utangazaji, lakini bado vituo vyetu havizingatii Kanuni na Sheria zilizopo. Kwa watu wanaoheshimu taaluma zao, sio jambo la kiungwana mamlaka zinazosimamia Sheria na Kanuni kuwakumbusha kila wakati nakuwachukulia hatua hivyo ni vyema kuheshimu taaluma kwa kufuataSheria na Kanuni zilizowekwa.

Alisema Kauli mbiu ya mkutano huo ni Wajibu wa vyombo vya Utangazaji kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 na kuwa kauli hiyo

inatukumbusha nafasi ya vyombo vyetu vya Utangazaji kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu mwezi Oktoba.

“Naomba nitumie nafasi hii kuvitaka vyombo vya Utangazaji kusimamiahaki na usawa katika kuhabarisha taifa mwenendo wa kampeni za vyama vya siasa pamoja na kuzingatia weledi na Kanuni za Utangazaji,” alisema Kabudi.

Wimbo wa Taifa ukiimbwa

Taswira ya mkutano huo.
Mkurugenzi wa Habarika Media, Shabani Lulela (kulia) akibadilishani mawazo na mshiriki mwenzake wa mkutano huo.
Wamiliki wa Online TV wakiwa kwenye mkutano huo.Picha ya pamoja na mgeni rasmi


No comments