Breaking News

MKUU WA MKOA WA TANGA AAINISHA MAFANIKIO YA MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Batilda Buriani

.......................................

Na Mwandishi Wetu, Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Batilda Buriani, ameupongeza uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan akisema uongozi wake umeambatana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake. Akizungumza na waandishi wa habari, Balozi Buriani alisema kuwa Serikali imefanya kazi kubwa kuimarisha miundombinu, huduma za kijamii, na kukuza uchumi wa mkoa huo, jambo ambalo limeleta maendeleo yanayoonekana kwa wananchi.

Mkuu huyo wa Mkoa amesemaa mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya miundombinu, ambapo barabara kuu na za vijijini zimeboreshwa, huku ujenzi wa madaraja na barabara za lami ukiendelea kuhakikisha usafiri unakuwa rahisi kwa wananchi bila kusahau upanuzi wa Bandari ya Tanga. 

Aidha amesema Serikali imewekeza katika kuboresha huduma za afya kwa kujenga na kukarabati hospitali, vituo vya afya, na zahanati, hivyo kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wakazi wa Tanga.

Katika sekta ya elimu, Balozi Buriani alieleza kuwa Serikali imefanikiwa kuongeza madarasa, kujenga shule mpya, na kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi. Kupitia mkakati wa elimu bila malipo, watoto wengi sasa wanapata fursa ya kusoma bila vikwazo, hatua inayosaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wanaoacha shule kwa sababu ya ukosefu wa ada na mahitaji mengine ya msingi.

Kwa upande wa uchumi na uwekezaji, Mkoa wa Tanga umeshuhudia ongezeko la miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo uwekezaji katika viwanda, kilimo cha kisasa, na uvuvi. Haya yote ni matokeo ya jitihada za Rais Samia katika kuvutia wawekezaji na kuhamasisha maendeleo ya sekta binafsi. Balozi Buriani alisisitiza kuwa kwa kasi hii ya maendeleo, Tanga inaelekea kuwa kitovu muhimu cha uchumi kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, huku wananchi wakifurahia matokeo chanya ya juhudi za Serikali. 

No comments