DC KILOSA: JESHI LA AKIBA NI NGUZO MUHIMU YA USALAMA NCHINI
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, akikagua gwaride wakati akifunga mafunzo miezi nne ya askari 114 mkupuo wa 20 wa Jeshi la Akiba yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mvumi wilayani humo Agosti 15, 2025.
.........................................
Na Dotto Mwaibale
MKUU wa Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Shaka Hamdu
Shaka amesema Jeshi la Akiba ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo wa usalama ndani
ya Taifa letu.
Shaka ameyasema hayo Agosti 15, 2025 wakati akifunga mafunzo ya miezi 4 ya askari
114 mkupuo wa 20 wa Jeshi la Akiba
yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya
Msingi Mvumi wilayani humo.
Alisema jeshi hilo kama alivyosema Luteni Kanali Ramadhani ni
sehemu ya akiba yetu muhimu pale ambapo itatokea dharura kwa kwenda kuunganisha
nguvu katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Nichukue nafasi hii kulishukuru Jeshi la Kujenga Taifa
Makao Makuu kwa kuratibu mafunzo haya na kuendelea kuwaandaa askari ili kuwa na akiba ya kutosha katika nchi yetu
na kujihakikishia usalama wetu hata pale litakapotokea tishio watanzania na
mipaka ya nchi yetu itabaki kuwa salama,” alisema Shaka.
Aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo kwenda kuzingatia maadili
na kuwa waaminifu kwa jamii kama walivyofundishwa na kuwa watatuzi wa
changamoto zao na kuifanya jamii kuendelea kuwa na umoja, upendo na mshikamano.
Shaka alisema Serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu
kwa muhitimu yeyote wa mafunzo hayo atakayeenda kufanya kinyume na kiapo
alichokiapa wakati wa kutumikia taifa na kueleza kuwa kiapo hicho kikawe
shuhuda kwao na kwa Mwenyezi Mungu.
Shaka alisema usalama wa nchi ni nguzo ya maendeleo na kuwa
wahitimu hao wanatakiwa kwenda kuimarisha nguzo hiyo kwa ajili ya mustakabaIi
wa taifa letu.
Alisema Wilaya ya Kilosa haipo kisiwani na kuwa
inachangamoto kadhaa kama za wananchi kujichukulia sheria mkononi, wizi wa
kuvunja, migogoro ya ardhi na nyingine nyingi hivyo ni wajibu wao kwenda
kusaidiana na vyombo vingine vya usalama na kuhakikisha wilaya hiyo inabaki kuwa
salama.
Aliwataka askari hao wa jeshi la akiba kwenda kushirikiana na vyombo vingine vya usalama wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu na kuhakikisha unafanyika kwa amani na utulivu.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, akihutubia wakati akifunga mafunzo hayo.
Wananchi wakishiriki hafla ya kufunga mafunzo hayo.
Askari wa Akiba wakiwa katika ufungaji wa mafunzo hayo.
Gwaride maalumu la askari wa akiba likipita mbele ya mgeni rasmi.
No comments