Breaking News

DORCAS MWILAFI WA CHADEMA ATIMUKIA CHAUMA, ACHUKUA FOMU YA UBUNGE JIMBO LA KAWE

Dorcas Francis Mwilafi ambaye alikuwa kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), Kinondoni Biafra Jijini Dar es Salaam leo Agosti 15, 2025 baada ya kuhamia chama hicho ambapo pia alichukua fomu ya kugombea Ubunge Jimbo la Kawe.

......................................

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

DORCAS Francis Mwilafi ambaye alikuwa kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa zaidi ya miaka 10 na kushika nafasi mbalimbali amekihama chama hicho na kutimkia Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) ambapo leo amechukua fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Kawe Jijini Dar es Salaam.

Mwilafi amepokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Benson Kigaila na kujinasibu kuwa atashinda na kuwa mbunge wa jimbo hilo.  

Mwanasiasa huyo mbobezi kabla ya kujiunga Chauma, akiwa Chadema amekuwa katika Nyanja za kisiasa na kushika nafasi mbalimbali kuanzia ngazi ya msingi, tawi, kata, jimbo hadi taifa.

Baadhi ya nafasi za uongozi ambazo alizihudumu akiwa Chadema ni Mjumbe wa  baraza la vijana, Mjumbe baraza la wanawake, mwenyekiti wa baraza la wanawake Kata ya Mbweni na katibu mtendaji wa jimbo la kawe, mgombea wa Bavicha Taifa, kuhudumu katika kamati tendaji ya kanda ya Pwani na nafasi nyingine mbalimbali za juu.

 “Chadema kimenipa uzoefu wa uongozi na wala siwezi kukisema vibaya kuja Chauma ni kuendeleza harakati zangu za kisiasa kupitia jukwaa lingine,” alisema Mwilafi.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Benson Kigaila akizungumzia mchakato wa kuchukua fomu kwa watia nia wote alisema fomu za tume ya uchaguzi zilianza kuchukuliwa jana lakini chama chao kinaratiba yao.

Alisema ratiba ya kuchukua ngazi ya urais ilianza Agosti 9, 2025 lakini kwa upande wa Chauma tarehe rasmi ya kuchukua fomu ya ngazi ya ubunge itakuwa ni Agosti 23 na 24 ndio zitakuwa tarehe za uteuzi.

Alisema baada ya uteuzi wa wagombea hao ndipo watatambulishwa kwa Tume ya Uchaguzi (INEC) ambapo watachukua fomu za kuomba kuteuliwa na tume hiyo lakini sasa hivi chama hicho kipo kwenye mchakato wa kutoa na kupokea fomu za watu wanaoomba wateuliwe.

Alisema tarehe ya mwisho kwa wanachama wa chama hicho wanaomba kugombea nafasi ya ubunge na udiwani ya kuchukua na kurejesha fomu hizo ndani ya chama ni leo saa 10 jioni.

Alisema tarehe ya uteuzi wa wabunge itafanywa na kamati kuu tarehe 23 na 24 mwezi huu na kuwa kabla ya hapo hawatakuwa na mgombea wa ubunge mpaka hapo atakapo teuliwa na kuwa sasa hivi wote ni watia nia.Dorcas Francis Mwilafi akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Benson Kigaila, akimkabidhi kadi ya uanachama Dorcas Mwilafi.Dorcas Mwilafi akionesha kadi baada ya kukabidhiwa.Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Benson Kigaila, akimkabidhi Dorcas Mwilafi fomu ya kugombea Ubunge Jimbo la Kawe.

Dorcas Mwilafi akionesha fomu ya kugombea ubunge baada ya kukabidhiwa.Dorcas Mwilafi akifurahi huku akionesha fomu ya kugombea ubunge baada ya kukabidhiwa.. Kutoka kushoto ni Mwana Chama wa Chauma, Prosper Makonya na Katibu wa Sekretarieti na Mkurugenzi wa Itikadi, Mafunzo na Elimu kwa Umma wa chama hicho, Edward Kinabo.

No comments